1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakosoa hukumu ya kifo kwa raia wake, Iran

22 Februari 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekosoa hukumu ya kifo iliyotolewa kwa Mjerumani aliye na asili ya Kiirani, Jamshid Sharmahd, akisema hukumu hiyo haikubaliki huku akiitaka Iran kuibatilisha.

https://p.dw.com/p/4NqPE
Protest gegen Hinrichtung im Iran
Picha: Willi Schewski/IMAGO

Kansela huyo wa Ujerumani amesema serikali ya Iran inatumia kila njia kupigana na watu wake wenyewe, bila kujali haki za binaadamu. Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter, Scholz ametoa wito kwa Iran kubatilisha mara moja hukumu hiyo iliyotolewa hapo jana.

Mapema hii leo, serikali ya Ujerumani iliwafukuza wanadiplomasia wawili katika ubalozi wa Iran mjini Berlin kufuatia hukumu hiyo dhidi ya raia wake huyo mwenye uraia pia wa Iran.

Scholz aushutumu uongozi wa Iran kwa kupigana na watu wake

Punde tu baada ya hukumu hiyo kutangazwa dhidi ya Jamshid Sharmahd, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Annalena Baerbock, alitoa taarifa ya kuwafukuza wanadiplomasia hao nchini Ujerumani. Kulingana na msemaji wa wizara hiyo wanadiplomasia hao wana siku chache za kufunga virago na kuondoka.

Katika taarifa yake, Baerbock aliitaka pia Iran kubatilisha uamuzi wake dhidi ya Sharmahd ili kutoa nafasi ya mshitakiwa kukata rufaa kwa kuzingatia utawala wa sheria. Jamshid Sharmahd, aliye na miaka 67, alitekwa nyara katika nchi ya kigeni na kulazimishwa kurejea Iran ili kujibu mashitaka yaliyokuwa yakimkabili.

Iran yasema Jamshid alihusika na shambulio la kigaidi

Iran | Deutsch-Iraner Djamshid Sharmahd in einem Teheraner Revolutionsgericht
Mjerumani mwenye uraia wa Iran, aliyehukumiwa kifo Jamshid SharmahdPicha: Koosha Falahi/Mizan/dpa/picture alliance

Tovuti ya Mahakama ya Kijeshi nchini Iran ya Mizan imesema Sharmahd alihusika na shambulio baya lililofanywa katika msikiti mmoja mwaka 2008 lililosababisha mauaji ya watu 14 huku wengine zaidi ya 300 wakijeruhiwa.

Anadaiwa pia kushirikiana na maafisa wa kijasusi wa Marekani na Israel na pia kuliongoza kundi la Tondar linaloshutumiwa kutaka kuuangusha utawala wa Iran. Kundi hilo limeorodheshwa kama kundi la kigaidi nchini humo.

Mwezi Agosti mwaka 2020 serikali ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu ilitangaza kumkamata Jamhshid Sharmahd raia wa Ujerumani ambaye pia ni mkaazi wa Marekani bila kutoa maelezo zaidi ya ni wapi alipokamatwa, lini hasa na katika mazingira gani. Lakini familia yake inasema alitekwa nyara alipokuwa Dubai na kupelekwa kinyume na matakwa yake nchini Iran.

Umoja wa Ulaya waiwekea Iran vikwazo vipya

Mtoto wake wa kike, Gazelle Sharmahd, ameendelea kusisitiza kuwa babake hana hatia na kutoa wito kwa Mataifa ya Umoja wa Ulaya kuishinikiza Iran kumuachia na kuokoa maisha yake. Amesema hali ya baba yake inaendelea kudhoofika, akiongeza kuwa "hana jino hata moja mdomoni na amenyimwa nafasi ya kuwaona watu wake, kwa hiyo hawajui yupo wapi na katika hali gani tangu alipoonekana mara ya mwisho."

Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Iran, IHR, lenye makao yake nchini Norway, Mahmood Amiry Moghaddam, ametoa wito wa jibu la pamoja la Ulaya dhidi ya hukumu hiyo aliyosema Iran inatumia kama silaha ya kisiasa. Amesema hatua iliyochukuliwa na Iran ni ya kujaribu kuighilibu Ulaya ili kupunguza shinikizo la kisiasa lililopo dhidi yake.

Chanzo: afp/dpa/reuters