Umoja wa Ulaya waiwekea Iran vikwazo vipya
21 Februari 2023Vikwazo hivyo vilivyotangazwa jana Jumatatu, vinatokana na jinsi nchi hiyo imewakandamiza waandamanaji, ambapo baadhi wamenyongwa.
Kwa jumla, vikwazo hivyo vinawalenga watu 32 na mashirika mawili. Miongoni mwa wale wamewekewa vikwazo hivyo ni waziri wa utamaduni ambaye pia hutoa maelekezo ya Kiislamu na vilevile waziri wa elimu.
Duru hiyo mpya ya vikwazo inaongeza idadi ya watu waliowekewa vikwazo nchini Iran kufikia 196 na mashirika 33. Hata hivyo, umoja huo haukupitisha pendekezo la kuliorodhesha jeshi la Walinzi wa Mapinduzi nchini humo kuwa kundi la kigaidi.
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema Umoja wa Ulaya hauna msingi wa kisheria kuliorodhesha jeshi hilo kuwa la kigaidi.
Iran imekumbwa na wimbi la maandamano katika miezi ya hivi karibuni, kufuatia kifo cha msichana aliyekuwa na umri wa miaka 22 Jina Mahsa Amini akiwa kizuizini mwa polisi.