Tunisia yakabiliwa na mgogoro mwingine wa kisiasa
16 Julai 2020Kujiuzulu kwa Elyes Fakhfakh katika nafasi yake ya Uwaziri Mkuu kumekuja wakati kukiwa na mgogoro wa kisiasa kati yake na chama cha Ennahda kutokana na mgongano wa maslahi.
"Ili kuepukana na migogoro katika taasisi kadhaa, waziri mkuu Elyes Fakhfakh amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa rais Kais Saied, ili kufungua njia ya kujiondoa katika migogoro hiyo," ilisema taarifa kutoka ofisi ya Fakhfakh.
Uhusiano kati ya waziri mkuu huyo anaeondoka mwenye umri wa miaka 47 na chama cha Ennahdha umekuwa ukiyumba tangu uchaguzi wa bunge wa mwezi Oktoba.
Fakhfakh, kiongozi wa chama kidogo cha social democratic amekuwa akichunguzwa na bunge kutokana na madai ya kushindwa kuwasilisha hisa anazomiliki katika kampuni binafsi iliyoshinda katika miezi ya hivi karibuni mkataba na serikali wa euro milioni 15.
Afisa Mkuu wa chama cha Ennahdha Abdelkarim Harouni ameuambia mkutano wa waandishi habari kuwa hali ya kiuchumi na kijamii ya Tunisia ni muhimu na inaweza kushughulikiwa na serkali ambayo uongozi wake haudhaniwi kuwa na mgongano wa mawazo.
Ushindi kwa Ennahdha
Kutokana na uamuzi huo rasi Saied wa Tunisia ana siku 10 tu za kumteua waziri Mkuu mpya. Chini ya Katiba ya Tunisia rais huyo ni lazima kwanza ajadiliane na vyama vya kisiasa kuhus yule atakayechukua nafasi hiyo na akishapatikana atakuwa na mwezi mmoja wa kupata uungwaji mkono wa bunge lililogawika.
Mapema hapo jana chama cha Ennahdha kiliwasiliha kura ya kutokuwa na imani na waziri Mkuu huyo aliyeingia madarakani mwishoni mwa mwezi February baada ya kuidhinishwa na bunge kufuatia miezi minne ya mkwamo wa kisiasa.
Katika uchaguzi wa mwezi Oktoba chama hicho kilishindwa kupata wingi wa kura bungeni baada ya kushinda viti 54 kati ya 217 vilivyopo, hatua iliyokilazimu kukubali kujiunga na serikali ya muungano.
Kulingana na mchambuzi wa kisiasa nchini humo Chokri Bahria, chama hicho kilikubali kuunda serikali ya muungano ili kuepuka kufanyika kwa uchaguzi mwengine mpya, lakini kikajikuta katika serikali ambayo hakina nguvu zaidi za kuidhibiti.
Kuondoka kwa Fakhfakh ni ushindi kwa chama cha ennahdha ambacho kimekuwa na mkwaruzano nae baada ya kukataa kukijumuisha chama mshirika kwa Ennahda katika serikali ya muungano.
Chama hicho kilimteua mgombea binafsi kuchukua nafasi ya waziri mkuu lakini kikashindwa kupata uungwaji mkono wa bunge hatua iliyomlazimisha rais kumteua waziri wa zamani Fakhfakh katika nafasi hiyo.
Tunisia ilijenga demkorasia yake baada ya maandamano ya mwaka 2011 yaliomuondoa rais wa muda mrefu na kuanzisha wimbi la maandamano katika mataifa ya Kiarabu.
Chanzo: afp,ap,dpa