Msimamo wa Chama Cha Ennahda Tunisia
10 Januari 2014Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tunisia, ni kuwa chama tawala cha Ennahda, kwa kutofautisha na washirika wao wa chama cha udugu wa kiislamu cha Misri, kilichochaguliwa madarakani baada ya machafuko ya mwaka 2011, na kupinduliwa na jeshi la nchi hiyo mwaka jana, wao wamefanikiwa kuondokana na migogoro ya kisiasa, na wameamua kung'atuka ili kuthibitisha uwepo wa amani katika kipindi cha mpito.
Chama hicho tawala nchini Tunisia, kimeamua kuachia madaraka kwa siku zijazo, kwa maafikino ya mkataba unaotaka kuundwa kwa tume ya uchaguzi na mpaka kufikia Tarehe 14 mwezi huu, mapendekezo ya mkataba wao yawe yamekwisha idhinishwa, kipindi ambacho watakuwa na maadhimisho ya tatu ya mapinduzi nchini humo.
Tangu mchakato wa katiba mpya ulipoanza wiki iliyopita, Chama cha Ennahda kimekubali kupunguza masuala mengi ya msimamo mkali wa kiislamu, na pia wamekubali msimamo wa uwepo wa haki za wanawake, na wamebaki na msimamo wa ahadi yao kuwa hawatofanya mashambulizi kwenye nyumba za kuabudu.
Matumaini ya kupitisha mkataba wa maridhiano ya kikatiba
Licha ya matukio kadhaa ya vurugu zilizokuwa zikitokea katika bunge la nchi hiyo, zaidi ya vifungu 40 kati ya150 vya katiba, mpaka sasa vimepitishwa kwa kura ya wengi, kitendo kinachoamsha matumaini kuwa, huenda theluthi mbili ya wabunge 217 waliochaguliwa wataidhinisha mkataba huo na kuepusha mapendekezo ya mkataba huo kuingizwa katika kura ya maoni.
Kwa mujibu wa mchambuzi mwingine binafsi wa masuala ya kisiasa, Selim Kharrat , anasema kuwa Chama cha Ennahda kilikubali kufanya baadhi ya mabadiliko ya masuala ya kisiasa na kuwa tayari kung'atuka kikiwa na nguvu kubwa, tangu miaka miwili iliyopita, baada ya kupata ushindi wa viti vingi katika bunge
Ennahda kutumia Demokrasia komavu
Wachambuzi wa kisiasa wanasema, mafanikio thabiti ambayo chama cha Ennahda kinaweza kuwa na matumaini nayo ni kutokana na kuridhia kwao suala la katiba, inayodokeza umuhimu wa kuimarisha uchumi na hali tete ya usalama wa nchi, inayosababishwa na uwepo wa vikundi vya dini vinavyopigana kwa kutumia silaha, ambapo kwa wakati huu chama cha Ennahda lazima kidhihirishie ulimwengu kuwa, viwango vya siasa za kiislamu vinaweza pia kulingana na viwango vya kimataifa vya demokrasia, hasa ukilinganisha tofauti yao na yale yanayoendelea katika mataifa mengine ya kiarabu yenye misimamo ya dini.
Mpaka sasa chama cha Ennahda kimefanikiwa pia kuwa waangalifu katika misimamo yao mikali na kuwafanya wakubaliane na maridhiano yaliyokuwa magumu kulingana na misimamo yao.
Kiongozi wa mstari wa mbele katika chama cha Ennahda, Habib Ellouze, alikemewa baada ya kumwita mwanasiasa mwenzake mwenye msimamo wa mrengwa wa shoto, kuwa ni adui wa uislam, tuhuma ambazo zilisababisha kuwepo kwa vitisho kadhaa vya kumuua mbunge huyo wa upinzani.
Marufuku kukashif uhuru wa watu kuabudu
Kutokana na kukabiliana na vitendo vya ukiukwaji wa misingi ya kiimani ndani ya bunge la nchi hiyo, chama hicho kimekubali pia ndani ya katiba yao kuwepo na pendekezo la kipengele cha sheria kinachozuia kumshutumu yeyote anayefanya shughuli za kichungaji. Hatua hiyo inadhihirisha jitihada zilizofanywa na chama cha Ennahda za kuheshimu maamuzi ya maridhiano waliyofanmya na wapinzani wao ingawaje wanachama wake waliochaguliwa ndani ya bunge ni hawajaungana.
Mtaalamu wa utamaduni wa kiislamu,Sami Brahem, hoja yake ni kwamba inaweza kusemekana kuwa chama cha Ennahda kinajionyesha kimekuwa cha kisasa kutokana na yale wanayofanya sasa, lakini ukweli ni kuwa kutokana na hali ya sasa ya kimaendeleo ya wa-Tunisia, kisingekuwa na uamuzi tofauti na walio nao sasa.
Hata hivyo kwa mujibu wa mwandishi wa habari za kisiasa wa gazeti la Le Quotidien, Mourad Sellami, ni kuwa chama cha Ennahda kimelazimika kulegeza misimamo waliyokuwa nayo baada ya kuona chama cha udugu wa kiislamu kilichokuwa na misimamo kama yao nchini Misri, kimeshindwa kuendelea kuongoza nchi ambapo jeshi la nchi hiyo lilipindua uongozi uliokuwepo na kuchukua madaraka tangu mwezi Julai mwaka 2013 mpaka sasa.
Jeshi la nchi hiyo lilipindua serikali ya Misri chini ya rais Morsi, baada ya kuuwawa kwa mbunge wa upinzani na raia kuamua kuingia mtaani na kufanya maandamano kwa siku kadhaa kupinga serikali iliyokuwepo.
Mwandishi: Diana Kago/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef