1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Tunisia wapiga kura kumchagua Rias mpya

Zainab Aziz Mhariri: John Juma
15 Septemba 2019

Raia wa Tunisia leo Jumapili watapiga kura kumchagua Rais mpya. Uchaguzi huo unatazamiwa kuwa ni kichocheo cha kukuza demokrasia kwenye nchi hiyo iliyotumbukia kwenye matatizo ya kiuchumi na matokeo ya vurugu.

https://p.dw.com/p/3PcnD
Tunesien Tunis - Wahlen
Picha: picture-alliance/AA/Y. Gaidi

Wagombea ishirini na sita wanawania katika uchaguzi huo, wa pili Tunisia wa kidemokrasia tangu yalipofanyika mapinduzi mnamo mwaka 2011 yaliyosababisha kuondolewa madarakani kiongozi wa muda mrefu Zine El Abidine Ben Ali.

Wagombea wakuu ni pamoja na Waziri Mkuu Youssef Chahed na Abdelfattah Morou naibu mkuu wa kundi la wanaharakati wa Kiislamu la Ennahda lenye ushawishi mkubwa nchini Tunisia. Mwingine ni mfanyabiashara maarufu Nabil Karoui, anayemiliki kituo cha televisheni na ambaye alikamatwa mwezi uliopita kwa tuhuma za utapeli wa pesa na ukwepaji kodi. Mahakama nchini Tunisia siku ya Ijumaa ilikataa ombi la kutaka Karoui anayezuiliwa aachiwe huru. Wafuasi wake wanasema tuhuma hizo zinalenga kumuharibia kisiasa mgombea wao.

Vile vile kwenye kinyang'anyiro hicho yupo Abdelkarim Zbidi aliyehudumu mara mbili kama waziri wa ulinzi, wakati wa utawala wa Beji Caid Essebsi. kwenye uchaguzi huu amesimama kama mgombea huru. Hapo jana, wagombea wawili walijitoa kwenye uchaguzi huo na kutangaza kwamba wameamua kumuunga mkono waziri huyo wa ulinzi.

Waziri Mkuu wa Tunisia Youssef Chahed
Waziri Mkuu wa Tunisia Youssef ChahedPicha: picture-alliance/Zumapress/C. Mahjoub

Wagombea wawili wanawake kwenye kinyang'anyiro hicho ni pamoja na waziri wa zamani wa utalii Salma Loumi na mwanasiasa Abeer Mousa, ambaye ni mpambe wa kiongozi wa muda mrefu aliyeng'olewa madarakani Zine El Abidine Ben Ali.

Uchaguzi huo wa Rais, uliopangiwa kufanyika mwezi Novemba, umesogezwa mapema baada ya Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Tunisia Beji Caid Essebsi, kufariki mnamo mwezi Julai, miezi mitano kabla ya kufikia mwisho wa kipindi chake.

Takriban wapiga kura milioni 7.2 wamesajiliwa kushiriki katika uchaguzi wa leo Jumapili. Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa mbili asubuhi na kuwa wazi kwa muda saa 10. Baada ya kura kuhesabiwa na iwe hakuna mshindi wa wazi basi itafanyika kura ya pili katika tarehe maalum ambayo bado haijatangazwa. Matokeo ya awali ya uchaguzi wa leo yanatarajiwa kutangazwa na tume ya uchaguzi wiki ijayo siku ya Jumanne.

Tunisia, ndio chimbuko la harakati na maadamano ya kutetea demokrasia ya 2010 na 2011 yaliyozikumba baadhi ya nchi za Afrika kaskazini. Maandamano hayo ya kupinga viongozi waliosalia madarakani kwa miongo kadhaa yanachukuliwa kuwa ni mafanikio ya kidemokrasia.

Vyanzo:/DPA/AFP