1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yafikiria vikwazo vya anga dhidi ya Libya

Halima Nyanza10 Machi 2011

Mataifa ya Ulaya bado yanajadili uwezekano wa kupitisha azimio la kuzuia ndege kutoruka juu ya anga ya Libya, huku mkutano wa dharura wa viongozi wa mataifa hayo ukitarajiwa kufanyika kesho (Ijumaa, 11 Machi 2011).

https://p.dw.com/p/10Wmu
Kamishna wa EU wa Nishati, Guenther Oettinger (kushoto)
Kamishna wa EU wa Nishati, Guenther Oettinger (kushoto)Picha: dapd

Uingereza na Ufaransa zimeendelea kuuchagiza Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kuzuia ndege kutoruka, kwa ajili ya kuzuia majeshi yanayomtii kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya watu wake.

Akizungumza katika bunge la Umoja wa Ulaya jana (Jumatano, 9 Machi 2011), Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja huo, Catherine Ashton, amewaonya wabunge wa Ulaya, kuendelea kuchukua tahadhari, akisema vikwazo na ushirikiano thabiti katika eneo hilo pia unazingatiwa.

Ashton amesema pia hakuna uamuzi wowote utakaochukuliwa mpaka pale viongozi wa Umoja huo watakapokutana katika kikao cha dharura kilichopangwa kufanyika kesho.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani. Thomas de Maiziere ameelezea kuwa na shaka na wazo la kuzuia ndege kuruka katika anga ya Libya na kusema kuwa mjadala wa wazi juu ya uamuzi huo si jambo la busara.

De Maiziere anataka mjadala wowote kuhusu vikwazo vya anga dhidi ya Libya ufanywe katika kiwango cha duru za usalama na sio kuwekwa hadharani kwenye vyombo vya habari.