Gaddafi azidisha mashambulizi dhidi ya waasi
9 Machi 2011Moshi mzito mweusi uliochanganyika na miale ya moto umeonekana kutanda katika anga la mji wenye mitambo ya mafuta wa Es Sider ulio mashariki mwa Libya leo hii (Jumatano 09.02.2011).
Bado hakuna chanzo huru cha habari kilichothibitisha nani aliyefanya mashambulizi hayo, lakini inafahamika kuwa, Es Sider ni miongoni mwa miji inayoshikiliwa na waasi, na ambapo vikosi vitiifu kwa Muammar Gaddafi, vimekuwa vikipigana kuirudisha mikononi mwa serikali.
Mpiganaji wa upande wa waasi, Abdel Salam Mohammed, ameliambia shirika hilo na hapa namnukuu: "Hapa tulipo tumesimama kwenye muelekeo wa Es Sider. Yalikuwa na mashambulizi makali ya mabomu dhidi yetu na kisha yakapiga matangi ya kuhifadhia mafuta."
Mpambe wa Gaddafi atua Cairo
Wakati hali ikiendelea hivyo ndani ya Libya, huko nchini Misri kuna ripoti kuwa mmoja wa watu wa karibu wa Gaddafi, Abdelrahman al-Zawi, amewasili uwanja wa ndege wa Cairo, huku mkutano wa mawaziri wa nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, ukitarajiwa kukutana mjini humo, kujadili uwezekano wa kuiwekea Libya vikwazo vya anga.
Bado haijulikani dhamira ya al-Zawi kutua ghafla nchini Misri, lakini huenda ni kuwasilisha ujumbe wa Gaddafi, ambaye hapo jana alionya kuwa, hatua yoyote ya kulifunga anga la Libya, itachukuliwa kuwa ni vita ambavyo nchi yake itavijibu inavyostahiki.
Hatua hiyo, ambayo pia inapigiwa chapuo na Uingereza, Ufaransa na Marekani, inatazamiwa kuzuia mashambulizi ya vikosi vya Gaddafi dhidi ya wapinzani wake, lakini haitoshi kuzuia umwagikaji damu unaoendelea nchini humo.
NATO haitaivamia Libya
Kwa upande mwengine, Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi, NATO, imesema kwamba haitarajii kuivamia Libya kijeshi, ingawa haikuondoa uwezekano wa hatua nyengine kutumika dhidi ya utawala wa Gaddafi.
Akizungumza na kituo cha habari cha Sky News cha Uingereza leo hii, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Fogh Rasmussen, amesema kwamba jumuiya yake haikusudii kujiingiza kijeshi nchini Libya, lakini iko tayari kuchukua hatua yoyote itakayostahiki, kama dharura ya kufanya hivyo itajitokeza.
"Ikiwa tutaombwa na ikihitajika, tunaweza kupatikana katika dharura hata ya muda mfupi. Kuna mambo mengi mazito katika eneo hili kuhusiana na uwezekano wa uingiliaji kati wa majeshi ya kigeni." Amesema Rasmussen.
Ujerumani yaamini vikwazo vya anga si njia pekee
Naye Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere ametaka mjadala wa kuwekwa marufuku ya ndege kuruka kwenye anga ya Libya kuchukuliwa kwa tahadhari, akisema kwamba hiyo ni moja tu kati ya hatua nyingi ambazo zinaweza kuchukuliwa, na wala sio hatua pekee.
Katika miaka ya 1990, jeshi la anga la Ujerumani lilikuwa sehemu ya operesheni inayolinda anga la Serbia dhidi ya ndege za kijeshi za Yugoslavia, hatua ambayo ilipingwa na watu wa Yugoslavia kama uingiliaji kati wa kigeni katika ardhi yao.
Akihofia hatima ya hatua hiyo, de Maiziere ameonya kwamba hatua zozote za kijeshi ni lazima zijadiliwe na viongozi wanaohusika na masuala ya usalama na sio kuwa mijadala ya wazi kwenye vyombo vya habari.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman