Gaddafi ayashutumu mataifa ya Magharibi kwa uasi
9 Machi 2011Katika mahojiano yaliyotangazwa leo kwenye televisheni ya taifa ya Libya, Muammar Gaddafi ameyashutumu waziwazi mataifa ya Magharibi kwamba ndiyo yaliyo nyuma ya uasi unaondelea sasa dhidi ya utawala wake na kuwaita Walibya wanaoshiriki kwenye uasi huu kuwa ni waasi.
"Mataifa ya kikoloni wanapanga njama za kuwadhalilisha watu wa Libya, kuwafanya watumwa na kuchukua mafuta yao." Amesema Gaddafi.
Katika mahojiano mengine mbali aliyofanya na kituo cha televisheni cha LCI cha Ufaransa, Gaddafi aliitaja kwa jina nchi ya Ufaransa kwamba iko kwenye mpango huo.
Ufaransa na Uingereza zimekuwa zikitoa wito wa kuwepo marufuku ya kuruka ndege kwenye anga ya Libya, ili kuzuwia vikosi vya Gaddafi visiwashambulie wapinzani kupitia angani. Hatua hii inaungwa mkono na Marekani, lakini kwa sharti la kuungwa mkono na kupitishwa na Umoja wa Mataifa.
Gaddafi awataka Walibya wawashinde waasi
Katika hatua nyengine, kituo cha televisheni ya taifa cha Libya, kimemuonesha Gaddafi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika mji wa Zintan, ulio umbali wa meli 75 kusini magharibi ya mji mkuu wa Tripoli, ambapo amewataka Walibya kuikomboa miji ya mashariki iliyochukuliwa na waasi.
Kwa mara nyengine, amelitaja kundi la Al-qaida, ambalo amesema linafanya kazi zake katika nchi za Misri, Algeria, Afghanistan na Mamlaka ya palestina kuwa ndilo linalohusika na machafuko yaliyoikumba Libya tangu katikati ya mwezi uliopita.
Majeshi ya Gaddafi yasonga mbele
Wakati haya yakiripotiwa, kuna taarifa kuwa vikosi vitiifu kwa kiongozi huyo vinaendelea na mashambulizi makali dhidi ya waasi. Mashahidi wanasema wameviona vifaru vya kijeshi vikikaribia mji wa Zawiyah ulio magharibi mwa Libya.
Akizungumza na Shirika la Habari la Reuters, mpiganaji mmoja wa upande wa waasi, aliyejuilikana kwa jina la Ibrahim, amesema kwamba vifaru vya wanajeshi wa Gaddafi vimezagaa kila kona za barabara kuu na za ng'ambo za mji huo wa Zawiyah, huku akitaja kuonekana kwa miili ya watu waliouawa na vikosi hivyo.
"Mji umeharibiwa kwa mashambulizi kutoka angani. Pia kuna watunguaji wenye silaha katika kila jengo refu, na wanampiga risasi kila anayejaribu kutoka nje. Hivi sasa kuna miili mingi ya watu barabarani na hatuwezi hata kuwazika. Zawiyah imehamwa. Huoni mtu mitaani. Hata wanyama. Hata ndege." Amesema Ibrahim.
Amesema kuwa kiasi ya wapiganaji wao 60 waliotoka kwenda kupambana na wanajeshi wa Gaddafi hapo jana, umbali wa maili 12 kutoka Zawiyah, hawakuwa wamerudi hadi sasa, na hawana uhakika ikiwa wako hai ama wameshauawa.
Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba, Libya imesimama njia panda, huku kukiwa hakuna hata upande mmoja kati ya pande znazopambana ambao una nguvu za kutosha kuushinda mwengine kwa sasa.
Kwa upande mmoja, vikosi vya Gaddafi havina uzoefu wa kupigana vita vya kukabiliana moja kwa moja, na kwa upande mwengine, waasi hawana silaha wala ujuzi wa kutosha kuweza kupambana na jeshi hadi ushindi.
Jambo hili linafanya kuwapo kwa uwezekano wa vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe, katika nchi ambayo bado utiifu kwa makabila ni mkubwa.
Hadi sasa jumuiya ya kimataifa haijakubaliana juu ya hatua za haraka kuchukuliwa kuzuia umwagikaji damu nchini Libya, huku wazo la kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya anga likisuasua.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/APE/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman