1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali bado tete Libya

7 Machi 2011

Wanajeshi watiifu kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, wameanzisha mashambulizi dhidi ya miji inayodhibitiwa na waasi.

https://p.dw.com/p/10UXz
Waasi wa Libya wakishangilia baada ya kuudhibiti mji wa Ras LanufPicha: AP

Hali hiyo inaongeza hofu kwamba nchi hiyo sasa inaelekea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na sio kufuata njia ya mapinduzi kama ilivyokuwa kwa Tunisia na Misri.Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amemtaka Kanali Gaddafi asitishe vitendo vya kuwashambulia raia, na kuonya kuwa yeyote atakayekiuka sheria za kimataifa atafikishwa mahakamani.

Hali nchini Libya inazidi kuwa tete baada ya vikosi vya wanajeshi watiifu kwa kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi, kuzidi kuelekea katika mji unaodhibitiwa na waasi wa Ras Lanuf ambao una utajiri wa mafuta, baada ya hapo jana kuudhibiti tena mji wa Bin Jawad uliopo eneo la mashariki. Hatua hiyo imesababisha wakaazi wa eneo hilo mapema leo asubuhi kuyakimbia makaazi yao kutokana na hofu kubwa inayozidi kutanda, huku Umoja wa Mataifa ukipeleka mjumbe wake mjini Tripoli na Marekani ikiwa katika shinikizo la kuwapatia silaha waasi wa Libya.

Hata hivyo, wakaazi hao wamesema baada ya mapigano makali hapo jana, Jumapili, yaliyohusisha kutupa makombora na kurusha roketi na mabomu, vikosi vya waasi vimetangaza kwamba vimewapiga wanajeshi watiifu kwa Gaddafi katika miji inayoidhibiti kwa sasa ya Zawiyah uliopo magharibi mwa Tripoli na Misrata uliopo kati ya Tripoli na Sirte. Wakaazi wa Misrata wamesema kuwa vifaru vya serikali vilirusha makombora katika mji huo na kuonya kuwa mauaji ya watu wengi yatafanyika iwapo jumuiya ya kimataifa haitaingilia kati.

Vereinte Nationen Ban Ki-moon Libyen
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: dapd

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amemtaka Kanali Gaddafi asitishe vitendo vya kuwashambulia raia na kuonya kuwa yeyote atakayekiuka sheria za kimataifa atafikishwa mahakamani. Bwana Ban ameyatoa matamshi hayo jana alipozungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Musa Kusa, ambapo alimwambia kuwa Libya haina budi kuwalinda raia wake. Aidha, Bwana Ban amemteua waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Jordan, Abdelilah Al-Khatib, kuwa mjumbe wake maalum atakayefanya mashauriano ya dharura na viongozi wa Libya na katika ukanda huo kuhusu hali ya kibinaadamu.

Katika hatua nyingine, Uingereza imesema kuwa timu ndogo ya wanadiplomasia imeondoka katika mji wa Benghazi, Libya, baada ya kujaribu kukutana na vikosi vya jeshi la upinzani, huku waasi wakiweka wazi kuwa wamekataa kufanya nao mazungumzo. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza, William Hague, alithibitisha jana kuwa ujumbe huo ulikwenda Libya kwa ajili ya kukutana na wapinzani, lakini sasa wameondoka Libya. Awali, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alielezea msimamo wao kwa Libya.

Waziri Mkuu Cameron alisema, ''Tutaendelea kuushinikiza utawala wa Libya, tutaendelea kueleza wazi sheria za kimataifa kuwa zimefika mbali na zina kumbukumbu ndefu na wale wanaofanya makosa dhidi ya ubinaadamu wataadhibiwa. Tutaendelea kutoa msaada wa kibinaadamu kwa wale walioathirika na mzozo huu na kuendelea kuyaomba mashirika ya misaada kuwafikia wale wanaohitaji msaada.''

Aidha, Waziri Mkuu huyo wa Uingereza alibainisha kuwa mkakati wao kwa Libya uko wazi, na kwamba wataendelea na mipango yao pamoja na washirika wao, lakini akasisitiza kuwa sasa umefika wakati kwa Gaddafi kuondoka madarakani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo(AFPE,RTRE,APE)
Mhariri: Miraji Othman