1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu zimezuka Libya

6 Machi 2011

Mapigano makali yamezuka kati ya waasi na vikosi vya serikali katika mji wa Zawiya uliopo magharibi mwa Libya, kiasi ya kilomita 50 magharibi mwa mji mkuu Tripoli.

https://p.dw.com/p/10U6h
Waasi na vikosi vya Gaddafi wote wadai ushindi mjini Zawiya.Picha: AP

Waasi walidai ushindi katika mji huo wa Zawiya. Lakini vikosi vinavyomuunga mkono Kanali Maummar Gaddafi waliwashambulia tena baadaye. Karim al Gawhary ni mwandishi habari aliyepo katika eneo la Benghazi, lililodhibitiwa na waasi.

Libyen Aufstände Proteste
Picha: AP

Idadi ya watu waliofariki kwenye mapigano hayo ya Zawiya haikujulikana mara moja, lakini wakaazi wanasema yalikuwa ni mauaji ya halaiki. Maafisa wa hospitali wamesema kiasi ya watu 30 wameuwawa katika mapigano ya awali mjini humo. Wakati huo huo, waasi hao sasa wanadai kuudhibiti mji uliopo pwani na ulio na utajiri wa mafuta, Ras Lanuf, jambo linalozidisha udhibiti wao wa maeneo yaliopo mashariki mwa nchi hiyo.

Upinzani Libya

Wakati huo huo vikosi vya upinzani nchini humo vimetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushinikiza marufuku ya ndege kutoruka katika anga za nchi hiyo. Baraza la kitaifa lililoundwa hivi karibuni linalonuia kutoa sura ya kisiasa kwa waasi wa kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi, pia walitoa wito wa kufungwa viwanja vya ndege kusini mwa nchi hiyo ambapo mamluki wanasemekana kuingia.

Libyen Evakuierung in Tripolis Flughafen
Raia wengi wamekusanyika katika uwanja wa kimataifa wa ndege Libya.Picha: AP

Baraza hilo la kitaifa linasema limekuwa likiwasiliana na balozi za nchi hiyo kote ulimwenguni kutafuta uungwaji mkono wa uasi huo. Kiongozi wake, aliyekuwa Waziri wa Sheria, Mustafa Abdel Jalil amekiambia kituo cha televisheni ya kiarabu ya Al Jazeera kuwa anatarajia nchi kadhaa za nje zenye nguvu kulitambuwa hivi karibini baraza hilo kama serikali halali ya mpito.

Mwandishi: Maryam Abdalla/ Dpa, Rtr
Mhariri:Grace Patricia Kabogo.