1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua ya Obama kwa Khamenei yazua mtafaruku

7 Novemba 2014

Vyombo vya habari Marekani vimesema rais Barack Obama, amemwandikia barua kiongozi wa kiroho wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, kuhusu vita dhidi ya Dola la Kiislamu, IS ambalo ni adui wa nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/1Dil4
Utawala wa Rais Obama umekataa kutoa maelezo ya ndani kuhusu barua yake kwa Ayatollah Khamenei
Utawala wa Rais Obama umekataa kutoa maelezo ya ndani kuhusu barua yake kwa Ayatollah KhameneiPicha: Reuters/Larry Downing

Ufichuzi wa kuwepo kwa barua hiyo ya Obama kwa Ayatollah Khamenei umekuja wakati muda wa mwisho wa mazungumzo kati ya Iran kwa Upande mmoja, na mataifa sita yenye nguvu duniani kwa upande mwingine, kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran wenye utata ukikaribia. Muda wa mwisho kwa mazungumzo hayo umewekwa tarehe 24 mwezi huu wa Novemba.

Gazeti la The Wall Street Journal lililoripoti kuhusu barua hiyo kwa mara ya kwanza, limesema ujumbe wa Obama kwa Ayatollah Khamenei unazungumzia maslahi ya pamoja kati ya Marekani na Iran katika vita dhidi ya kundi la IS. Hata hivyo kwa mujibu wa gazeti hilo, Obama alisisitiza kwamba ushirikiano wowote katika vita hivyo utategemea kupatikana kwa makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Ikulu yakwepa ufafanuzi

Ikulu ya Marekani, White House haikutaka kutoa maelezo ya kina kuhusu barua hiyo, lakini msemaji wake Josh Earnest amewaambia waandishi wa habari kwamba utawala wa rais Obama hauna mpango wowote wa kushirikiana na Iran kijeshi.

Kiongozi wa kiroho wa Iran, Ayatollah Khamenei ndie mwenye kauli ya mwisho nchini humo
Kiongozi wa kiroho wa Iran, Ayatollah Khamenei ndie mwenye kauli ya mwisho nchini humoPicha: khamenei.ir

''Siwezi kuzungumza juu ya mawasiliano kati ya rais na viongozi wengine ulimwenguni. Ninachoweza kuwaelezeni ni kwamba sera ya utawala huu wa rais Obama kuhusu Iran inabakia pale pale: Tunazungumza kuhusu mpango wake wa nyuklia ili kuondoa wasi wasi wa dunia, lakini hatushirikiani kijeshi, wala kubadilishana taarifa za kijasusi.'' Amesema Earnest.

Lakini wakosoaji wakubwa wawili wa sera za raia Obama, seneta John McCain kutoka jimbo la Arizona, na Lindsey Graham wa Calorina ya Kusini wamesema wamestushwa na hatua hiyo ya nadra ya rais Obama kuijongelea Iran, nchi ambayo ni mshirika mkubwa wa rais wa Syria Bashar al-Assad na inayounga mkono makundi ya kishia yenye misimamo mikali katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati.

''Matokeo ya juhudi hizi mbaya ni kuharibu nafasi yoyote kwa wasyria kuweza kujinasua katika utawala wa rais Assad na kuishi kwa uhuru'', limesema tangazo lililotolewa kwa pamoja na maseneta hao.

Bado hakuna dalili za mwafaka

Maafisa wa Marekani hawajaondoa uwezekano kwamba kufikiwa kwa makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kunaweza kufungua milango ya ushirikiano katika masuala mengine, lakini wamejaribu kuyabakiza mazungumzo ya sasa juu ya suala hilo tu la nyuklia ya Iran.

Uhusiano wa kidiplomasia Kati ya Iran na Marekani ulivunjwa baada ya mapinduzi ya mwaka 1979 nchini Iran,
Uhusiano wa kidiplomasia Kati ya Iran na Marekani ulivunjwa baada ya mapinduzi ya mwaka 1979 nchini IranPicha: monazereh.ir

Nafasi ya mafanikio katika mazungumzo hayo bado siyo ya uhakika. Akizungumza Jumatano wiki hii, rais Obama alisema uwezekano wa kupatikana mwafaka ni swali ambalo bado halina jibu.

Wadau katika mazungumzo hayo ambao ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi, China na Ujerumani, wamekuwa kimya kabisa kuhusu maendeleo ya mchakato wa mazungumzo hayo.

Marekani na Iran zilivunja uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1979, baada ya mapinduzi ya kiislamu nchini Iran na kuvamiwa kwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran na kukamatwa raia 52 wa Marekani ambao walishikiliwa mateka kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Mwandishi: APE/DPAE

Mhariri:Josephat Charo