1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry kuzungumza na Obama juu ya Iran

Mjahida15 Julai 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema atajadili na Rais Barrack Obama uwezekano wa kurefusha muda uliowekwa wa kufikia makubaliano juu ya nyuklia za Iran, unaomalizika mwezi huu.

https://p.dw.com/p/1CdaE
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters

Akizungumza mjini Vienna baada ya siku mbili za mazungumzo ya kina na Waziri mwenzake wa Iran Mohammad Javad Zarif, Kerry amesema licha ya kupiga hatua katika mazungumzo hayo bado kuna mapengo halisi katika masuala mengine ya msingi.

"Kama nilivyosema tumepiga hatua, na kuna kazi bado ya kufanya. Kwa hiyo tuangalie kipi kitafanyika kwa siku na saa zijazo. Iwapo nitaombwa kurejea tena hapa nitarejea lakini sina mipango ya kufanya hivyo ninapoondoka kwenda Washington kujadiliana na rais," alisema Kerry.

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amesema, atakaporejea Washington atazungumza na rais Barrack Obama na viongozi wengine wa Congress kuhusu makubaliano ya dhati na hatua za baadaye, iwapo hawatafanikiwa kufikia makubaliano ifikapo Julai 20.

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Iran Mohammed Zarif na mwenzake John Kerry
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Iran Mohammed Zarif na mwenzake John KerryPicha: Getty Images

Muda unayoyoma wa kufikia makubaliano

Julai 20 ni siku ambayo makubaliano ya muda yakufikia suluhu ya mpango wa nyuklia wa Iran, yaliowekwa kati ya nchi hiyo na mataifa matano ya kudumu katika baraza la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujermani yanamalizika, hii ikimaanisha kuwa makubaliano mengine ya mwisho yanapaswa kufikiwa kabla ya wakati huo.

Hatua ya kurefusha muda wa mwisho wa makubaliano ni jambo linalowezekana ili kutoa nafasi ya mazungumzo zaidi kati ya mataifa husika, lakini Marekani imesema haitakubaliana na hilo iwapo hapatakuwa na maelewano ya mwanzo kabisa kutoka taifa hilo la kiislamu.

Mataifa ya Magharibi yamekuwa na wasiwasi kuwa Iran ina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia jambo ambalo Iran inaendelea kukanusha na kusema mpango wake ni kwaajili ya amani, lakini ikasema pia ina haki ya shughuli za nyuklia chini ya makubaliano ya Kimataifa.

Wataalamu wa silaha za nyuklia
Wataalamu wa silaha za nyukliaPicha: Imago

Mazungumzo haya yanafanyika huku Iran ikiwa na matumaini ya kuondolewa vikwazo ilivyoekewa na Umoja wa Mataifa pamoja na Mataifa ya Magharibi, vinavyoyumbisha uchumi wake.

Mataifa hayo sita yalio na nguvu duniani, Ufaransa, Urusi, Marekani, Uingereza, China na Ujerumani yanaitaka Iran kuachana na mpango wake wa nyuklia kwa muda mrefu na kukubali wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuuchunguza mpango huo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul- Rahman