Kerry aahidi kuisaidia Iraq
23 Juni 2014Kerry alikutana na Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki miongoni mwa mikutano atakayokuwa nayo na viongozi wa kisiasa na kijamii nchini Iraq.
Kerry amewaambia waandishi wa habari mjini Baghdad kwamba msaada wa Marekani utakuwa mkubwa na wa kuendelezwa na iwapo viongozi wa Iraq watachukuwa hatua zinazohitajika kuiunganisha nchi hiyo msaada huo utakuwa wa manufaa.Amesema Iraq inakabiliwa na hatari kubwa sana.
Ziara yake inakuja baada ya wanamgambo hao wa Kisunni kunyakuwa maeneo ya ngome zao kuu kwenye mpaka wa magharibi wa Iraq mwishoni mwa juma na kuimarisha njia za kupitishia misaada na silaha kutoka Syria ambapo wameutumia kwa manufaa yao uasi wa miaka mitatu nchini humo kuteka maeneo mengi ya Iraq.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Jen Psaki amesema Kerry atazungumzia hatua za Marekani kuisaidia Iraq wakati ikikabiliana na tishio hilo na kuwahimiza viongozi wa Iraq kuharakisha mchakato wa kuunda serikali itakayowakilisha maslahi ya wananchi wa Iraq.
Rais Barack Obama wa Marekani alikubali wiki iliopita kutuma kikosi maalum cha wanajeshi 300 kama washauri lakini Marekani imesita kufanya mashambulizi ya anga na kufuta uwezekano wa kutuma wanajeshi wake wa ardhini nchini humo.
Serikali yazidi kuchochea uasi
Serikali ya Marekani ina wasi wasi kwa serikali ya al-Maliki inayoongozwa na Washia imezidi kuuchochea uasi huo kwa kuwatenga Wasunni wa msimamo wa wastani ambao walipambana na kundi la Al Qaeda na hivi sasa wamejiunga na uasi huo wa kundi la wapiganaji wa Kisunni la Dola la Iraq na Sham ISIL.
Kerry amesema hapo jana kwamba Marekani haitomteua au kuchaguwa nani anayepaswa kuongoza Iraq hata hivyo amesema serikali yake imeona kuwepo na hali ya kutoridhika miongoni mwa Wakurdi, Wasunni na baadhi ya Washia kutokana na uongozi wa al- Maliki na kusisitiza kwamba Marekani inataka wananchi wa Iraq wawe na uongozi ambao uko tayari kukubali ushirikishi na kushirikiana madaraka.
Iraq ilitarajiwa kuunda serikali mpya baada ya uchaguzi wa mwezi wa April ambapo wagombea wa al-Maliki walishinda viti vingi bungeni lakini lakini bado wanahitaji washirika wa kuweza kuwa na wingi wa viti bungeni.
Maliki na madaraka
Maafisa wa Marekani wamedokeza kwamba wako tayari kuona Maliki anaondoka madarakani.Wanasiasa waandamizi wa Iraq akiwemo mmoja wa chama tawala cha Maliki ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba ujumbe huu umewasilishwa kwa njia ya lugha ya kidiplomasia kwa viongozi wa Iraq.
Hapo jana kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Al Khamenei ameishutumu Marekani kwa kujaribu kuirudisha tena Iraq mikononi mwake baada ya kuikalia kwa mabavu huko nyuma madai ambayo Kerry ameyakanusha kwa kusema kwamba Marekani imejitolea kuisaidia Iraq lakini inataka kuwepo kwa serikali itayokuwa shirikishi zaidi.
Hapo jana wanamgambo wamekiteka kituo cha pili cha mpakani kwenye mpaka wa Syria wakiendeleza harakati zao za wki mbili za kuteka maeneo zaidi kwa lengo la kuunda utawala kuanzia Syria hadi Iraq jambo ambalo limezusha fadhaa Mashariki ya Kati na mataifa ya magharibi.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters/AFP
Mhariri : Josephat Charo