Marekani kuzungumza na Iran kuhusu Iraq
16 Juni 2014Waziri Kerry amesema pia katika mahojiano na mtandao wa habari wa Yahoo, kwamba ndege za mashambulizi zisizo na rubani huenda zikatumiwa. Alipoulizwa juu ya uwezekano wa kushikriana na Iran, waziri Kerry amesema haondowi uwezekano wa jambo lolote lenye manufaa, lakini akasisitiza kuwa mawasiliano yoyote na Iran yatakwenda hatua kwa hatua.
Maafisa wa Marekani walisema hapo awali, kuwa kuna uwezekano kuwa naibu waziri wa mambo ya kigeni William Burns akaizungumza hali nchini Iran na ujumbe wa Iran wakati wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran mjini Vienna. Utawala wa Obama pia unatafakari mashambulizi ya upande mmoja ya angani ili kupunguza kasi ya uasi unaoitishia serikali ya waziri mkuu Nouri al-Maliki.
Kila liwezekanalo
Waziri Kerry alisema njia hizo siyo jawabu kamili ya mgogoro unaoendelea nchini Iraq, lakini zinaweza kuwa mmoja ya njia muhimu kwa sasa kuzima wimbi hilo la uasi na kuzuwia mienendo ya wapiaganaji wanaozunguka kwenye malori wakiwatishia na kuwauwa watu.
Wakati mji mkuu Baghdad ukikabiliwa na kitisha cha kusonga mbele kwa wapiganaji, wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imeimarisha usalama kwenye ubalozi wa Marekani na kuwaondoa baadhi ya wafanayakazi wake nje ya mji huo. Katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO Anders Foghs Rassmussen ambaye alikuwa nchini Uturuki leo amazungumzia pia hali nchini Iraq.
"Tunayafuatlia matukio ya hatari nchini Iraq kwa wasiwasi mkubwa. Nalaani mashambulizi yasiyokubalika dhidi ya ubalozi mdogo wa Uturuki mjini Mosul, na nataka kuwachia mara moja kwa raia wa Uturuki waliotekwa pamoja na maafisa usalama," alisema Rassmusen baada ya kufanya mkutano na rais wa Uturuki Abdulah Gul.
Uingereza yazungumza na Iran
Serikali ya Uingereza nayo imesema leo kuwa waziri wake wa mambo ya kigeni William Hague ameuzungumzia mgogoro wa Iraq na mwenzake wa Iran Mohammad Javad Zarif, kukiwa na ripoti kuwa Tehran inatafakari kutoa msaada wa kijeshi kwa utawala wa waziri mkuu Maliki.
Ofisi ya mambo ya kigeni ya Uingereza ilikataa kutoa maelezo zaidi juu ya mazungumzo ya simu kati ya Hague na Zarif, lakini waziri Hague alitarajia kulitaarifu bunge jioni ya leo. Mapema, waziri Hague alisisitiza kuwa Uingereza haitaingilia kijeshi kuisaidia Iraq kupambana na wapiganaji, ambao wameyateka maeneo makubwa ya nchi hiyo katika kipindi cha siku tu.
Hague alikanusha madai kuwa hali ya vurugu inayoendelea nchini Iraq ilikuwa matokeo ya moja kwa moja ya uvamizi wa Marekani na Uingereza mwaka 2003, ambao ulimuondoa madarakani rais Saddam Hussein, ingawa alikiri kuwa makosa yalifanyika baada ya uvamizi huo.
Mwandishi. Iddi Ssessanga/afpe,ape
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman.