1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Walemavu wa kusikia kujitokeza kupiga kura Senegal

Saleh Mwanamilongo
7 Machi 2024

Nchini Senegal, wapiga kura walio na ulemavu wa kusikia wanatafuta njia ya kupiga kura, huku taifa hilo la Afrika Magahribi likisubiri kwa hamu uchaguzi wa rais ambao umepangwa kuitishwa Machi 24.

https://p.dw.com/p/4dHFx
Watu wanaoishi na ulemavu wa kusikia wapewa mafunzo ya upigaji kura nchini Senegal
Watu wanaoishi na ulemavu wa kusikia wapewa mafunzo ya upigaji kura nchini Senegal Picha: Sadak Souici/AP Photo/picture-alliance

Kama ilivyo kwa wengi katika jamii ya walio na ulemavu wa kusikia nchini Senegal, Mame Massar Faye mwenye umri wa miaka 52 amekuwa akijitahidi kupiga kura peke yake. Amesema mara nyingi ilikuwa vigumu kwake kufanya hivyo. Faye amesema alikuwa akipiga kura miaka ya nyuma kwa usaidizi wa mkalimani wa lugha ya ishara, kwa sababu kila wakati alilazimika kuomba msaada.

Bwana huyo kutoka mji wa Thies amesema alikuwa kifanya hivyo mara nyingi pasina kuelewa baadhi ya masharti  fulani yanayohusiana na mchakato wa kupiga kura.

Huku Senegal ikikabiliana na mzozo baada ya uchaguzi wa rais kucheleweshwa, wengi katika jamii ya walionaulemavu wa kusikia wanajiandaa kupiga kura kwa usaidizi wa kifaa kipya cha uchaguzi.

Lakini hata hivyo kuna changamoto kwa watu hao, Senegal haina lugha ya ishara inayofanana, huku jamii ikitumia mchanganyiko wa Lugha ya Ishara ya kienyeji, Kiarabu na lugha nyingine za kimataifa.

''Huuliza maswali mara kwa mara''

Alioune Sow, mwenyekiti wa shirikisho la kitaifa la mashirika ya walionamatatizo ya kusikia nchini Senegal (FNOSS) amesema kutokana na hali hiyo, baadhi ya taarifa zinazohusiana na mchakato wa upigaji kura hazitumiki sana au hazieleweki.

''Vijana wengi walionaulemavu wa kusikia wanapiga kura kwa mara ya kwanza. Kwa mafunzo haya, waliokuwepo walielewa mchakato wa upigaji kura. Lakini bado kuna wengi ambao hawajapata taarifa muhimu. Kwa hiyo mimi binafsi nitawaeleza hawa walio na ulemavu wa kusikia jinsi ya kupiga kura. Nitajaribu kusambaza video na maelezo niliyopokea wakati wa mafunzo. Watu walio na ulemavu wa kusikia huuliza maswali mara kwa mara kuhusu uchaguzi.", alisema Faye.

Msamiati wa kujadili siasa

Walemavu wanyanyapaliwa katika jamii na mara nyingi hawapewi fursa ya elimu
Walemavu wanyanyapaliwa katika jamii na mara nyingi hawapewi fursa ya elimuPicha: Cem Ozde/Anadolu/picture alliance

Orodha ya maneno 105 katika lugha ya ishara ya Senegal kuanzia karatasi ya kupigia kura na kituo cha kupigia kura ilitayarishwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Kimataifa la Mifumo ya Uchaguzi IFES kwa ushirikiano na mashirika kadhaa ya kitaifa.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha kabla ya uchaguzi wa rais wa Senegal, wapiga kura walio na ulemavu wa kusikia watashiriki msamiati mmoja kujadili siasa na kujifunza nini cha kufanya siku ya uchaguzi itakapofika. Faye ametoka kushiriki katika warsha inayofundisha orodha ya masharti, ambayo anasema hatimaye itamruhusu kupiga kura peke yake bila usaidizi.

Ukusanyaji data sahihi juu ya jamii ya walio na ulemavu wa kusikia nchini Senegal ni changamoto, lakini Aloune Sow alisema wamekusanya takriban asilimia mbili ya idadi ya watu hao mnamo 2022. Idadi kubwa wamekataliwa kupiga kura ama kwa sababu hawajui la kufanya siku ya uchaguzi, au pia kwa sababu ya ukosefu wa wakalimani katika ofisi za manispaa au vituo vya kupigia kura.

Walemavu wanyanyapaliwa katika jamii

Mame Faye ambaye ni fundi cherehani na mwenyekiti wa watu walio na ulemavu wa kusikia mjini Thies amesema watu hao wengi wanahitaji kufundishwa kuelewa jinsi ya kupiga kura. Amesikitishwa kuona kwamba mara nyingi habari hutolewa kwenye runinga na redio bila mkalimani.

Pia, kutengwa katika jamii kunachangiwa na ukweli kwamba wengi hawapelekwi shule, hiyo inamaanisha kwamba hawawezi kusoma nyenzo za kampeni au maagizo ya kupiga kura.