Mkanganyiko kuhusu tarehe rasmi ya uchaguzi Senegal
7 Machi 2024Tangazo la kuitishwa uchaguzi hapo Machi 24 limetolewa baada ya kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika Jumatano jioni, ambapo pia Rais Macky Sall aliivunja serikali na kumteua waziri wa mambo ya ndani, Sidiki Kaba, kuwa waziri mkuu.
Hata hivyo, bado kuna mkanganyiko kuhusu tarehe rasmi ya duru ya kwanza ya uchaguzi, baada ya Mahakama ya Katiba ya Senegal, kusema kuwa uchaguzi huo unapaswa kufanyika Machi 31.
Kwa sasa haijajulikana ni siku gani hasa uchaguzi huo utaitishwa. Katiba ya Senegal inampa mamlaka rais kutangaza tarehe ya kuitishwa uchaguzi, lakini katiba hiyo hiyo inasema uamzi wa Mahakama ya Katiba hauwezi kupingwa na mamlaka yoyote nchini.
''Sall anamachaguo mawili pekee''
Djibril Gninggue, mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa la Asasi za Kiraia kwa Uchaguzi wa Uazi nchini Senegal amesema Rais Macky Sall hana chaguo lolote hivi sasa bali kuachia madakara ifikapo April 2.
''Mahakama ya Katiba lilithibitisha uamuzi wake wa Februari 15. Kwa hivyo Rais Sall ana machaguo mawili pekee: ama afanye uchaguzi kabla ya Aprili 2 au abaki hadi Aprili 2 na kuondoka. Katika ngazi ya kisheria, haya ni machaguo mawili ambayo amebakisha.''
Daftari ya wagombea 19 wa urais
Kabla ya tangazo la Jumatano, viongozi walikuwa wamejaribu kuahirisha uchaguzi wa awali wa Februari 25 hadi Desemba, uamuzi uliosababisha machafuko makubwa mitaani.
Baadaye mazungumzo ya kitaifa yaliyosusiwa na baadhi ya wanasiasa yalipendekeza uchaguzi ufanyike Juni 2 na kwamba Macky Sall asalie madarakani hadi mrithi wake atakapoteuliwa. Lakini Mahakama ya Katiba ya Senegal ililikataa pendekezo hilo.
Katika uamuzi tofauti hapo jana, Mahakama hiyo ya Katiba pia ilisema kinyang'anyiro cha urais kinapaswa kujumuisha orodha ya wagombea urais 19 ambao tayari wameidhinishwa na chombo hicho. Uamuzi huo ni pigo jingine kwa Rais Sall ambaye alipendekeza kuwajumuisha wagombea wengine kwenye daftari ya uchaguzi wakiwemo Karim Wade na Ousmane Sonko, ambao walikuwa wamezuiwa kushiriki.
Sheria ya msamaha
Huku hayo yakijiri, wabunge jana usiku walijadili na kupitisha muswada tata wa msamaha unaohusu vitendo vinavyohusishwa na maandamano ya kisiasa katika miaka ya hivi karibuni.
Senegal ilishuhudia matukio kadhaa ya machafuko mabaya kati ya 2021 na 2023, yaliyochochewa hasa na mzozo mkali kati ya kiongozi wa upinzani aliyefungwa sasa, Ousmane Sonko, na serikali.
Wachambuzi wanaamini kwamba hatua za serikali, mahakama na bunge za hapo jana ni msukumo wa kweli kwa mchakato wa uchaguzi wakati Senegal inapitia mzozo mkubwa kabisa wa kisiasa ambao haujawahi kutokea tangu kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais.