Waislamu milioni 1 wahudhuria ibaada ya Hajji Mecca
4 Julai 2022Mabango ya kuwakaribisha waumini, wakiwemo wageni wa kwanza wa kimataifa tangu 2019, yamepamba viwanja na mitaa, huku vikosi vya usalama vilivyojihami vikishika doria katika mji huo wa kale, alikozaliwa Mtume Muhammad.
"Hii ni furaha tupu," mhujaji wa Sudan Abdel Qader Kheder aliiambia AFP mjini Makka, kabla ya tukio hilo kuanza rasmi Jumatano. "Karibu siamini kuwa nipo hapa. Ninafurahia kila wakati."
Watu milioni moja, wakiwemo 850,000 kutoka nje ya nchi, wanaruhusiwa katika hajj ya mwaka huu baada ya miaka miwili ya idadi iliyopunguzwa sanakutokana na janga la corona. Hijja ni moja ya nguzo tano za Uislamu, ambayo Waislamu wote wenye vigezo na uwezo wanatakiwa kuitekeleza angalau mara moja katika maisha yao.
Soma pia: Karibu milioni mbili wahudhuria Hijja Makka
Siku ya Jumatatu alasiri, mahujaji wakiwa wamebeba miavuli kujikinga na jua kali walimiminika kwenye maduka ya kumbukumbu na vinyozi huko Makka, huku wengine wakishiriki milo chini ya mitende kwenye mitaa iliyo karibu na Msikiti Mkuu.
Mahujjaji wengi wapya walikuwa tayari wameanza kufanya ibada ya kwanza, ambayo inahitaji kutembea mara saba kuzunguka Kaaba, ambayo ni jengo kubwa la rangi nyeusi katikati ya Msikiti Mkuu.
Kaaba ambayo ilitengenezwa kwa matale na kufunikwa kwa kitambaa chenye aya za kutoka Korani takatifu, ina urefu wa karibu mita 15 (futi 50). Ndiyo sehemu ambako Waislamu wote wanaelekea kusali, bila kujali walipo duniani.
"Nilipoiona Kaaba kwa mara ya kwanza nilihisi kitu cha ajabu na nikaanza kulia," Hujaji wa Misri Mohammed Lotfi aliiambia AFP. Takriban mahujaji 650,000 wa kigeni wamewasili Saudi Arabia hadi sasa, walisema maafisa wa serikali siku ya Jumapili.
Mnamo mwaka wa 2019, takriban watu milioni 2.5 walishiriki katika ibaada hiyo, ambayo pia ni pamoja na kukusanyika kwenye Mlima Arafat na "kumpiga mawe shetani" huko Mina.
Soma pia: Mamilioni ya Waislam wanaanza ibada ya Hajj Makka
Mwaka uliofuata, wakati janga hilo lilipoanza, wageni walizuiliwa na waumini walipunguzwa hadi 10,000 tu kuzuia ibaada hiyo kugeuka kuwa msambazaji mkuu wa virusi ulimwenguni. Idadi hiyo iliongezeka hadi 60,000 kwa raia na wakaazi wa Saudi waliochanjwa kikamilifu mnamo 2021.
Mahujaji mwaka huu -- ambao ni walio na umri wa chini ya miaka 65 pekee -- watashiriki katika hajj chini ya masharti magumu ya usafi.
Hija imeshuhudia maafa mengi kwa miaka mingi, ikiwa ni pamoja na mkanyagano wa 2015 ambao uliua hadi watu 2,300 na shambulio la 1979 na mamia ya watu wenye silaha, ambalo kulingana na idadi rasmi, lilisababisha vifo vya watu 153.
Chanzo kikubwa cha fahari
Hija ni chanzo chenye nguvu cha ufahari kwa utawala wa kifalme wa kihafidhina wa taifa la jangwani la Saudi Arabia, na mtawala wake mkuu, Mwanamfalme Mohammed bin Salman, ambaye anarejea kutoka jangwa la kidiplomasia.
Siku chache baada ya ibada ya hijja, Mwanamfalme Mohammed atamkaribisha Rais wa Marekani, Joe Biden ambaye, kutokana na kuzidi kupanda kwa bei ya mafuta kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, amekengeuka kiapo chake cha kuigeuza Saudi Arabia kuwa taifa lililotengwa kutokana na mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi mwaka 2018 na mawakala wa Saudia.
Ibaada ya Hajji, ambayo inagharimu kiasi kisichopungua dola 5,000 kwa kila mtu, ni njia ya kuvuna fedha kwa taifa hilo linalouza mafuta kwa wingi duniani inajaribu kuleta uchumi wake mseto. Katika miaka ya kawaida hija huingiza mabilioni ya dola.
Soma pia: Mahujaji waanza ibada ya Hajji mjini Makka
Pia ni fursa ya kuonyesha mabadiliko ya haraka ya kijamii ya ufalme huo, licha ya malalamiko yanayoendelea kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na mipaka ya uhuru wa kibinafsi.
Saudi Arabia -- ambayo chini ya mageuzi ya hivi majuzi imeruhusu rafu huko Riyadh na fukwe za watu wa jinsia tofauti huko Jeddah - sasa inaruhusu wanawake kuhudhuria ibada ya hijja bila kusindikizwa na jamaa wa kiume, hitaji ambalo lilitupiliwa mbali mwaka jana.
Masharti ya covid yalegezwa
Barakoa siyo lazima tena katika sehemu nyingi za ndani nchini Saudi Arabia lakini zitakuwa za lazima katika Msikiti Mkuu, eneo takatifu zaidi katika Uislamu. Mahujaji kutoka nje ya nchi watalazimika kuwasilisha matokeo ya vipimo vya covid-19 yaani PCR.
Msikiti Mkuu "utaoshwa mara 10 kwa siku... na wafanyakazi zaidi ya 4,000 wa kiume na wa kike", na zaidi ya lita 130,000 (galoni 34,000) za dawa ya kuua vijidudu hutumika kila wakati, walisema maafisa.
Tangu kuanza kwa janga hili, Saudi Arabia imesajili zaidi ya kesi 795,000 za mambukizo ya corona, vifo 9,000, katika idadi ya watu wapatao milioni 34.
Soma pia: Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia afariki
Kando na Covid, changamoto nyingine ni jua kali katika moja ya kanda zenye joto na ukame zaidi ulimwenguni, ambalo linazidi kuwa mbaya zaidi kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Ingawa majira ya kiangazi ndiyo kwanza yameanza, halijoto tayari imepanda nyuzi joto 50 (122 Fahrenheit) katika sehemu za Saudi Arabia.
Lakini hujjaji wa Iraq Ahmed Abdul-Hassan al-Fatlawi alisema joto ni jambo la mwisho analofikiria akiwa Makka.
"Nina umri wa miaka 60, kwa hivyo ni kawaida ikiwa nitachoka kimwili kwa sababu ya hali ya hewa ya joto, lakini niko katika hali ya utulivu, na hilo ndilo jambo muhimu kwangu," aliiambia AFP.