Karibu milioni mbili wahudhuria Hijja Makka
9 Septemba 2016Athari za maafa hayo yaliyosababishwa na mkanyagano zimechangia mzozo mpya kati ya Saudi Arabia na hasimu wake wakikanda Iran, ambayo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu miongo mitatu haijapeleka watu kuhijji. Wakati nguzo kuu za tukio hilo la siku sita zinaanze leo Jumamosi, tayari mahujaji wamekuwa wakiizunguka kaaba katika msikiti mkuu wa Makka, katika msururu unaoendelea mchana na usiku.
Ni mmoja ya nguzo za kwanza ha hajji, ambayo ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya watu duniani. Hajji ni moja ya nguzo tano za Uislamu, ambayo Waislamu wenye uwezo walapaswa kutekeleza angalau mara moja maishani. Matajiri na maskini kwa pamoja wanakuja wakiwa wamevalia nguo sawa nyeupe.
"Sina hofu yoyote," alisema Adil Abdulrahman, hujjaj kutoka Uingereza akiwa na imani kwamba mamlaka zimejaribu kuwafanya waumini wajisikie salaama. Mgeni kutoka Nigeria, Lawan Nasir, alisema kumpoteza binamu yake katika mkanyagano wa mwaka jana hakukumzuwia kushiriki Hijja ya mwaka huu. Nasir alisema maumivu ya kufiwa ndugu yake hayajapungua, lakini akaongeza kuwa lingekuwa jambo upumbavu kutokuja.
Usalama waimarishwa
Katika mmoja ya hatua ya kiusalama zilizochukuliwa baada ya mkanyagano wa mwaka jana, uingiaji katika eneo la kaaba ambako Waislamu wanaelekea wakati wanaswali kutoka sehemu zote za dunia, umezuwiwa wakati wa swala, na pia matembezi ya kuizunguka ili kuzuwia mrundikano wa watu.
Gazeti la serikali ya Saudi jana Ijumaa liliwanukuu maafisa wa msikiti wakisema eneo la kuzungukia limepanuliwa ili kuweza kuchukuwa mahujjaji elfu 30 kwa saa, idadi hii ikiwa imepanda kutoka 19,000. Usalama umeimarishwa pia kuzunguka eneo hilo takatifu zaidi la dini ya Kiislamu, kwa kuweka maafisa zaidi wanalinda usalama katika vizuwizi vya kijani ili kuwadhibiti watu.
Wakati wa swala ya Ijumaa hapo jana umati wa watu waliovalia nguo nyeupe ulilifanya eneo linalozunguka kaabda kuonekana kutokea juu kama uwanja uliongukiwa na theluji. helikopta ilikuwa ikifanya doria juu na barabara kuu katika mji huo zilifungwa kuruhusu mamia kwa maelfu ya watembea kwa miguu kuweza kufika.
Vikuku vya utambulisho
Huku joto likiwa katikakiwango cha nyuzi 43 za celsius, baadhi ya mahujjaji walionekana kuchoka. Walibeba maji na kujaribu kusaidiana chini ya jua kali. Serikali ya Saudi ilianza kutoa vikuku vya utambulisho kwa mahujaji, baada ya baadhi ya maafisa wakigeni kuelezea wasiwasi juu ya ugumu katika kuwatambua wahanga wa mkanyaganyo.
Kila kikuku kina bar code inayosomeka kwa kutumia simu ya kisasa aina ya Smartphone. Kinaonyesha utambulisho wa hujjaj, utaifa wake, mahala anakolala mjini Makka, na pia taarifa nyengine. Naibu waziri wa wizara ya masuala ya hijja na Umra Issa Rawas, alisema lengo la vikuku hivyo ni kuwandaa mahujjaji wa kigeni, ambao wanatarajiwa kuwa zaidi ya milioni 1.4. Vyombo vya habari vya ndani ya Saudi Arabia vinasema zaidi ya waumini laki tatu kutoka ndani ya taifa hilo la kifalme walitarajiwa kushiriki ibada ya Hijja.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Saumu Yusuf