1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Wafaransa wapiga kura duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge

7 Julai 2024

Raia wa Ufaransa wanapiga kura leo Jumapili katika duru ya pili ya uchaguzi wa bunge ambao yumkini utakipatia ushindi wa kihistoria chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally (RN).

https://p.dw.com/p/4hyqi
Ufaransa | Uchaguzi | Bunge
Raia wa Ufaransa akipiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa bunge unaofanyika 07.07.2024.Picha: Jean-Francois Badias/AP Photo/picture alliance

Chama hicho kinachoongozwa bungeni na mwanasiasa Marine Le Pen kinapendelea sera za kizalendo na kuyaweka mbele maslahi ya Ufaransa kwanza na vilevile kinapinga suala la uhamiaji.

Uchaguzi wa leo utaamua iwapo RN itanyakua majimbo mengi au Ufaransa itapata bunge ambalo hakuna chama chenye udhibiti kamili.

Uchaguzi huo utakuwa na taathira siyo ndani ya Ufaransa pekee bali pia kimataifa. Mathalani utaamua kuhusu hatma ya msaada ambao Ufaransa inautoa kwa Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi na uthabiti wa kiuchumi kwenye kanda ya Umoja wa Ulaya.

Marine Le Pen wa chama cha National Rally
Marine Le Pen wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Rally. Picha: Jerome Domine/abaca/picture alliance

Ufaransa imo kwenye ukingo wa kupata serikali ya kwanza ya mrengo mkali wa kulia tangu vikosi vya Manazi vya Ujerumani vilipoikamata na kuikalia nchi hiyo kwa mabavu wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Iwapo RN kitashinda wingi mkubwa wa vita bungeni kiongozi wake Jordan Bardella atakuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Vitimbi vyashuhudiwa wakati wa kampeni tofauti na desturi za Wafaransa 

Masuala ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wayahudi viligubika kampeni za uchaguzi pamoja na kampeni za Urusi kupitia mitandao.

Zaidi ya wagombea 50 waliripoti kushambuliwa kitu ambacho ni nadra katika siasa za Ufaransa. Serikali imesambaza askari 30,000 kupiga doria na kusimamia usalama kwenye uchaguzi wa leo.

Ufaransa | Emmanuel Macron | Uchaguzi
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.Picha: Aurelien Morissard/Pool/AP Photo/picture alliance

Upigaji kura ulioanza kwenye maeneo yaliyo chini ya milki ya Ufaransa tangu kusini mwa bahari ya Pasifiki hadi kwenye kanda ya Karibia, bahari ya Hindi na kaskazini mwa bahari ya Atlantiki.

Upigaji kura utamalizika saa kumi na mbili jioni kwa saa za Ufaransa.

Matarajio ya awali ya matokeo ya uchaguzi huo yataanza kutolewa usiku wa loe na ifikapo kesho Jumatatu matokeo kamili yatakuwa yamepatikana.

Waziri Mkuu Gabriel Attal amepiga kura kwenye kitongoji cha Vanves kilicho kwenye mji mkuu wa Ufaransa, Paris.

Rais Emmanuel Macron alitarajiwa kupiga kura kwenye mji wa mwambao wa La Touquet wakati Le Pen hatopiga kura baada ya kushinda jimbo lake la uchaguzi kaskazini mwa Ufaransa wiki iliyopita.