Vikosi vya Ukraine vyasonga mbele ndani ya ardhi ya Urusi
8 Agosti 2024Katika chapisho lake la hivi karibuni, taasisi hiyo ya utafiti wa vita imesema vikosi vya Ukraine vimethibitishwa kusonga mbele hadi kilomita 10 katika jimbo la Kursk la Urusi huku operesheni za uchokozi zikiendelezwa kwenye eneo la Urusi.
Taasisi hiyo imeongeza kuwa hatua hiyo ya vikosi vya Ukraine kuingia katika eneo la Urusi inaonyesha kuwa vikosi hivyo vimepenya angalau safu mbili za ulinzi za Urusi na ngome yake kuu.
Jeshi la Urusi lathibitisha uvamizi wa Ukraine
Kulingana na jeshi la Urusi, vikosi vinavyoiunga mkono Ukraine, vilivamia eneo la Kursk kusini-magharibi mwa Urusi siku ya Jumanne asubuhi, na kuwapeleka karibu wanajeshi 1,000 na zaidi ya magari ya vita na mizinga 24.
Soma pia:Mashambulizi nchini Urusi yaharibu dhana ya 'jeshi la Putin'
Jenerali mkuu wa jeshi nchini Urusi, aliapa jana Jumatano kukabiliana na uvamizi huo na kuwarudisha nyuma wapiganaji hao wa Ukrainehadi kwenye mpaka.
Uvamizi huo umejikita kwenye mji wa Sudzha, ulio na takriban wakaazi 5,000 na ulioko umbali wa kilomita nane kutoka mpaka wa Ukraine.
Ukraine yapiga hatua kubwa katika vita vyake na Urusi
Hakujakuwa na maelezo zaidi kutoka kwa maafisa wa Urusi, lakini wanablogu wa kijeshi wa Urusi, wanaoshirikiana na jeshi hilo, pia wameripoti kuwa Ukraine imepiga hatua kubwa na pia wakalalamika kuhusu kuzorota kwa hali.
Soma pia:Ukraine/ Russia: Yanayoendelea katika vita vya nchini Ukraine tangu ilipovamiwa na majeshi ya Urusi
Katika ujumbe katika mtandao wa Instagram, mwanablogu mmoja Yury Podolyaka amesema hali ni ngumu na inaendelea kuwa mbaya zaidi.
Podolyaka ameongeza kuwa mji huo wa Sudzha umejaa wanajeshi wa Ukraine.
Jeshi la Urusi laharibu gari la vita la Ukraine
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa vikosi vyake vimeharibu gari la vita aina ya Bradley lililotengenezwa Marekani ambalo Ukraineilikuwa ikitumia katika uvamizi huo na kwamba pia imeangusha droni za Ukraine katika eneo hilo.
Gavana wa Kursk atangaza hali ya dharura
Hapo jana jioni, gavana wa eneo hilo la Kursk alitangaza hali ya dharura hatua ambayo inaipa mamlaka uwezo wa kudhibiti shughuli za watu na kutuliza hali iliyopo.
Hata hivyo Ukraine haijatoa maoni rasmi kuhusu operesheni hiyo.
Kampuni ya mafuta ya Urusi ya Gazprom kusafirisha mafuta kupitia Ukraine
Huku hayo yakijiri, kampuni kubwa ya mafuta ya Urusi Gazprom, imesema leo kuwa itaendelea kusafirisha gesi kupitia kituo cha Sudzha, kituo cha mwisho cha kupitisha gesi ya Urusi kuelekea Ulaya kupitia Ukraine.
Mshukiwa wa ''uhaini'' Urusi huenda akakabiliwa na kifungo cha miaka 15 jela
Waendesha mashtaka nchini Urusi wameomba hukumu ya kifungo cha miaka 15 jela kwa mtu mmoja anayeshikilia uraia wa mataifa mawili ya Urusi na Marekani, Ksenia Karelina anayeshtakiwa kwa "uhaini" kwa kutoa mchango kwa shirika linaloiunga mkono Ukraine.
Soma pia:Putin anatabasamu licha ya shinikizo
Mashirika ya habari ya serikali, leo yamemnukuu wakili wa Karelina, Mikhail Mushailov akithibitisha kuwa upande wa mashtaka uliomba hukumu hiyo ya kifungo cha miaka 15 jela katika gereza moja la kikoloni.