1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasema huenda ikaishambulia Ukraine

Mjahida 14 Julai 2014

Urusi inafikiria hatua ya kujibu mashambulizi dhidi ya Ukraine baada ya raia wake kuuwawa kufuatia kombora lililovurumishwa nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/1CcWh
Mmoja wa wanajeshi wa Urusi
Mmoja wa wanajeshi wa UrusiPicha: AFP/Getty Images

Gazeti hilo la kila siku limesema Urusi inafikiria uwezekano wa kuanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi, dhidi ya Ukraine ambapo mapambano kati ya waasi wanaoiunga mkono Urusi na vikosi vya serikali, vikizidi kupamba moto na kutishia kugeuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

"Uvumilivu wetu haumaanishi kuwa tumefikia kikomo," Alisema afisa aliyekaribu na ikulu ya Urusi ya Kremlin, aliyenukuliwa na gazeti moja la kila siku la Kommersant. la Urusi. Ameongeza kuwa Urusi inafahamu ni wapi yanakorushwa makombora kutoka Ukraine na kwamba wanania ya kulenga mahala hapo pekee.

Mabomu kadhaa yalifyatuliwa ndani ya kijiji kidogo cha urusi cha Donetsk kilicho na jina sawa na eneo linaloshikiliwa na waasi wanaotaka kujitenga Mashariki mwa Ukraine. Shambulizi hilo lilisababisha mtu mmoja kuuwawa na wengine wawili wakijeruhiwa.

Rais Petro Poroschenko
Rais Petro PoroschenkoPicha: SERGEI SUPINSKY/AFP/Getty Images

Msemaji msaidizi wa baraza la juu la bunge la Urusi, Yevgeny Bushmin, alisema wanahitaji kutumia silaha zenye malengo maalum kama inavyofanya Israel, ikiwa ni pamoja na kuwaangamiza wale wanaofanya hujuma hizo. Jana wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi ilikielezea kisa hiki kuwa ni uchokozi kutoka Ukraine unaoweza kuwa na matokeo ya kudumu.

Hata hivyo Ukraine imekana kutekeleza shambulizi hilo huku ikisema kuwa haijawahi na haitawahi kurusha kombora katika eneo jirani.

Mgogoro Mashariki mwa Ukraine ulianza mwezi wa Aprili wakati wapiganaji wenye silaha wanayoiunga mkono Urusi walipodhibiti miji na majengo ya serikali wiki kadhaa baada ya rais Victor Yanokovich kuondolewa madarakani. Aidha mapigano yamezidi kupamba moto katika siku za hivi karibuni baada ya vikosi vya Ukraine kuwasukumu nyuma waasi nje ya mji wa Slaviansk.

Yanoukovich afungua kesi ya kupinga vikwazo dhidi yake

Wakati huo huo rais wa zamani wa Ukraine Viktor Yanukovych, amefungua kesi katika mahakama ya Juu ndani ya Umoja wa Ulaya ya kupinga vikwazo alivyowekewa pamoja na watoto wake wawili wa kiume.

Mahakama hiyo ya Umoja wa Ulaya imeiorodhesha kesi ya Yanoukovich pamoja na kesi ya viongozi wengine mashuhuri katika mgogoro wa Ukraine, ulioanza wakati rais huyo wa zamani alipokataa kuwa na mahusiano ya karibu zaidi na Umoja wa Ulaya hatua iliosababisha maandamano dhidi yake, na baadaye kuondolewa madarakani.

Miongoni mwa wale waliofungua kesi katika mahakama hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine Mykola Azarov na mwanawe wa kiume.

Rais wa Zamani wa Ukraine Viktor Yanukovych
Rais wa Zamani wa Ukraine Viktor YanukovychPicha: Reuters

Mwezi Machi, Umoja wa Ulaya ulimuekea vikwazo Yanukovych pamoja na washirika wake wa karibu ikijumuisha kuzuiwa kwa mali zao kutokana na madai ya rushwa.

Kwengineko viongozi wengine wa Urusi nao pia wameekewa vikwazo sawa na hivyo pamoja na kunyimwa kusafiri kutokana na majukumu yao katika mgogoro unaoendelea nchini Ukraine.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman