1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi, mataifa ya Ulaya zapanga mpango wa amani wa Ukraine

7 Februari 2015

Viongozi wa Urusi, Ujerumani na Ufaransa wamekubaliana katika mazungumzo yao mjini Moscow kupanga mpango wa kumaliza mapigano nchini Ukraine wakati waasi wakifanya mashambulizi makubwa upande wa mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1EXYe
Merkel und Hollande zu Gesprächen mit Putin in Moskau
Mkutano wa pande tatu, kansela Merkel (kushoto) Francois Hollande(kulia) na Vladimir Putin (katikati)Picha: picture-alliance/epa/S. Ilnitsky

Msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kuwa zaidi ya saa nne za mazungumzo ambayo yamekamilika mapema leo alfajiri yameshuhudia viongozi hao wakikubaliana kuhusu mswada wa waraka maalum ambao pia utajumuisha mapendekezo kutoka kwa Rais wa Ukraine Petro Poroshenko.

Ankunft Merkel und Hollande zu Gesprächen mit Putin in Moskau
Wakati wa kuwasili viongozi wa Ulaya mjini MoscowPicha: Reuters/S. Karpukhin

Hakuna maelezo zaidi ya mpango huo yaliyotolewa, lakini msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov amewaambia waandishi habari mazungumzo hayo yamekuwa ya "maana na yenye tija" na kuongeza kwamba Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Francois Hollande waliondoka mara baada ya mazungumzo hayo.

Matayarisho yamo mbioni

"Kazi imo mbioni kutayarisha waraka wa uwezekano wa waraka wa pamoja kutekeleza makubaliano ya Minsk," amesema Peskov, akimaanisha makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwezi Septemba ambayo yamekuwa yakikiukwa kwa kiasi kikubwa.

Deutschland Russland Merkel zu Besuch in Moskau
Kansela Merkel akiwasili mjini MoscowPicha: Reuters/Sergei Karpukhin

Afisa wa Ufaransa pia ameyaita mazungumzo hayo "ya maana na yenye kuleta matarajio" na kusema kazi inaendelea kutayarisha nyaraka za pamoja zenye lengo la kutekeleza makubaliano hayo ya mwezi Septemba ya kusitisha mapigano.

Putin, Merkel na Hollande , ambao hawakuzungumza na vyombo vya habari baada ya mkutano wao, watajadili juhudi hizo na Rais wa Ukraine Petro Poroshenko kwa simu kesho Jumapili (08.02.2015).

Mazungumzo hayo ya viongozi hao wawili wa Ulaya pamoja na kiongozi wa Urusi yanaonekana kuwa ni juhudi za kuzuwia mzozo huo uliodumu kwa miezi 10 sasa mashariki mwa Ukraine kufikia hatua ya kutoweza kudhibitiwa wakati Marekani inatafakari kuipelekea silaha serikali ya Ukraine.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Kansela Merkel nchini Urusi tangu ulipozuka mzozo wa Ukraine wakati Hollande alifanya ziara fupi mwezi Desemba.

Ukraine Kiew Merkel Poroschenko Hollande
Mkutano kati ya kansela Merkel , Francois Hollande na Petro Poroshenko wa Ukraine.Picha: Reuters/V. Ogirenko

Kabla ya mazungumzo hayo, Merkel alizungumzia matumaini madogo ya kumalizika haraka kwa mapigano ambayo yamesababisha zaidi ya watu 5,300 kupoteza maisha tangu mwezi Aprili mwaka jana.

Lakini aliongeza: "Tunapaswa kufikisha mwisho umwagaji huu wa damu na kutekeleza makubaliano ya Minsk." Merkel na Hollande kwanza walikwenda Kiev siku ya Alhamisi kwa majadiliano, wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry pia alikuwa akifanya ziara katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev.

Kerry na Lavrov kukutana

Kerry anatarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov katika mkutano wa usalama mjini Munich leo Jumamosi(07.02.2015), wakati wana diplomasia wa ngazi ya juu wakitafuta kuutatua mzozo mbaya kabisa kati ya mataifa ya mashariki na magharibi tangu kumalizika kwa vita baridi.

John Kerry zu Besuch in Pakistan 12.01.2015
John Kerry waziri wa mambo ya kigeni wa MarekaniPicha: Reuters/R. Wilking

Jana Ijumaa, makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden amesema Ukraine inapambana kwa ajili ya kujinusuru kutokana na kuongezeka kwa kujihusisha kwa jeshi la Urusi katika mzozo huo.

"Sisi, Marekani na Ulaya kwa jumla, tunapaswa kusimama pamoja na Ukraine katika wakati huu," Biden amesema mjini Brussels.

Joe Biden bei Donald Tusk
Joe Biden makamu wa rais wa MarekaniPicha: Reuters/F. Lenoir

"Urusi isiruhusiwe kuchora upya ramani ya Ulaya. "Rais Putin anaendelea kutoa wito wa mipango mipya ya amani wakati majeshi yake yanaingia nchini Ukraine, na anapuuzia kabisa kila makubaliano ambayo nchi yake imetia saini hapo kabla," Biden ameongeza.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri : Caro Robi