Uturuki yaunga mkono azma ya Ukraine kujiunga na NATO
8 Julai 2023Akizungumza katika mkutano wa pamoja mjini Istanbul, Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan amemwambia rais Zelensky kwamba Ukraine bila shaka inastahili uanachama wa NATO.
Kauli hii inajiri kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wa muungano huo wa kijeshi, utakaofanyika Jumanne wiki ijayo, huko Vilnius Lithuania.
Zelensky ni miongoni mwa viongozi watakao hudhuria mkutano huo na hivi karibuni alisema alitarajia mwaliko rasmi wa nchi yake kujiunga na NATO. Hata hivyo Marekani ilididimiza matuamini ya Ukraine kwa kusema mkutano huo hautafikia maamuzi hayo kwa haraka.
Nchi za NATO zimekuwa na mjadala juu ya ni lini hasa na ni jinsi gani Ukraine inaweza kuwa mwanachama na katika mazingira gani. Wanachama kama vile Ujerumani wanasisitiza kwamba masharti fulani ni lazima yatimizwe, ikiwa ni pamoja na jeshi kuwa chini ya udhibiti wa kiraia na kidemokrasia.