1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Namibia wapinga makubaliano ya Fidia ya Ujerumani

23 Septemba 2021

Wakati wa mchakato wa majadiliano katika bunge la Namibia, wabunge wa upinzani wamekosoa mpango wa fidia wa euro bilioni 1.1 wa Ujerumani kwa mauaji ya halaiki yaliofanywa mwaka1904-1908 dhidi ya jamii ya Herero na Nama

https://p.dw.com/p/40lFU
Namibia Windhoek | Proteste gegen Genozid Abkommen mit Deutschland
Picha: Sakeus Iikela/DW

Mwezi Mei mwaka huu serikali ya Namibia ilisema Ujerumani ilikubali kufadhili miradi ya maendeleo nchini humo kwa miaka 30 kama njia moja wapo ya kuomba msamaha na kurekebisha makosa yaliofanyika zaidi ya karne moja iliyopita wakati maelfu ya raia wa namibia walipouwawa kwa kukiuka masharti ya ukoloni wa Ujerumani.

Lakini vyama vya upinzani na viongozi wa kitamaduni nchini humo kutoka jamii zilizoathirika za Herero na Nama wamekasirishwa na kitita kilichokubalika wakisema ni kidogo mno na hawakuhusishwa katika majadiliano kati ya serikali hizo mbili.

soma zaidi: Bunge la Namibia kujadili makubaliano ya fidia ya Ujerumani

Siku ya Jumanne waandamanaji 300 waliyavamia majengo ya bunge la Namibia wakati makubaliano ya fidia yalipowasilishwa.

Esther Muinjangue, rais wa chama cha upinzani cha NUDO amesema kuwa makubaliano yaliyopo hayaelezei au kuzingatia masuala yao, yanazungumzia kuhusu mauaji ya halaiki na fidia na ujenzi upya, lakini kile wanachokitaka sio ujenzi upya wa Namibia, ukweli ni kwamba Ujerumani imetekeleza mauaji ya halaiki na ni lazima ilipe fidia, anasema hicho ndicho wanachokitaka.

Upinzani wataka kitita cha euro bilioni 9 kama fidia

Namibia, Windhuk I Denkmal zur Erinnerung an den Völkermord von Herero und Nama
Picha: Jürgen Bätz/dpa/picture alliance

Kiongozi mwengine wa upinzani wa chama cha RDP Mike Kavekotora, amesema serikali ya Namibia inapaswa kupata angalau kitita cha cha euro bilioni 9 kutoka Ujerumani kama fidia kwa mateso yaliofanyika dhidi ya jamii hizo mbili.

Kwa upande wake waziri wa ulinzi Frans Kapofi wa chama tawala cha SWAPO amekiri kuwa makubaliano hayo hayawasilishi matarajio yote ya jamii husika lakini tayari majadiliano yameshafanyika.

Amesema lengo la serikali kuu ya Namibia ni kutaka Ujermani kukubali kuwa wanajeshi wake walitekeleza mauaji ya halaiki. Majadiliano yanaendelea hii leo kabla ya makubaliano hayo kupigiwa kura na huenda yakapita kutokana na chama tawala SWAPO kuwa na wingi wa kura bungeni.

soma zaidi: Bunge la Namibia lajadili maridhiano na Ujerumani

Muwakilishi wa serikali ya ujerumani katika mji mkuu wa Namibia Windhoek hakuweza kupatikana kutoa maoni yake juu ya mchakato huo bungeni.

Wakati wa vita vya Herero na Nama kuanzia mwaka 1904 hadi 1908, kulikuwa na mauaji ya halaiki yanayochukuliwa kama mauaji ya kwanza ya aina hiyo katika karne ya ishirini. Wanahistoria wanakadiria kwamba Waherero 65,000 kati ya 80,000 na Wanama 10,000 kati ya 20,000 waliuwawa.

Chanzo: afp