1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Kenya wasisitiza kuendelea na maandamano

Thelma Mwadzaya16 Machi 2023

Wanasiasa wa upinzani nchini Kenya wamesisitiza kuendelea na maandamano ya kitaifa yatakayohitimishwa Jumatatu ijayo jijini Nairobi wakiwa na madai kadha wa kadhaa, ikiwemo kupanda kwa gharama za maisha.

https://p.dw.com/p/4Oji5
Kenia Präsidentschaftswahl | Raila Odinga
Picha: John Ochieng/Zuma/IMAGO

Tayari kiongozi wa upinzani wa chama cha Orange Democratic Movement, ODM, Raila Odinga ameitangaza tarehe 20 ya mwezi huu na kuwa siku ya mapumziko ili wakenya waweze kushiriki kwenye maandamano hayo.

Tamko hilo limezua mitazamo tofauti kwani halina msingi wa kisheria.

Alasiri ya leo waandamanaji walikusanyika kwa amanimjini Kisumu ambako wameahidi kukutana tena siku ya Ijumaa wanapojiandaa kwa mhadhara wa kilele uliopangiwa mwanzo wa wiki ijayo.

Kwa mujibu wa naibu gavana wa kaunti ya Kisumu, Mathew Owiti ,maandamano ya maandalizi ni ya siku mbili ili kuitikia wito wa kiongozi wa upinzani wa ODM, Raila Odinga.

Soma pia:Kenya kuendesha oparesheni kusaka majangili

Kiongozi wa chama cha NARC-Kenya ambacho ni sehemu ya muungano wa Azimio Martha Karua anasisitiza kuwa dawa ni maandamano ili kudai haki kwa wakenya.

Hii leo, baraza kuu la makanisa nchini Kenya liliunga mkono maandamano ya Jumatatu ijayo ya tarehe 20 kwa msingi kuwa gharama za maisha zimeongezeka mno na wakenya wanaumia.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, mwenyekiti wa baraza hilo la NCCK kanda ya Nyanza Bishop David Kodia alifafanua kuwa serikali ya Kenya Kwanza inaonekana kushindwa nguvu na haina uwezo wa kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Kwa upande wake,baraza la waislamu nchini Kenya,SUPKEM, linapinga maandamano hayo ya kuishinikiza serikali kwani hayataleta tija.

Mataifa mengine yafanya maandamano sawa na hayo

Maandamano ya Jumatatu ijayo yaliyopangwa kufanyika jijini Nairobi yatafanyika siku moja na mengine kwenye mataifa 4 barani Afrika.

Kenia Nairobi | Raila Odinga und Unterstützer
Raila Odinga kiongozi wa upinzani KenyaPicha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Nchini Nigeria,wanasiasa wa upinzani wameitisha maandamano ya kutilia mkazo mjini Lagos kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mwezi uliopita.

Mjini Tunis, yamepangwa maandamano ya kupinga utawala wa kiimla wa rais Kais Saied wa nchi ya Tunisia.

Waandamanaji wa upinzani wamekuwa wakikusanyika mjini Tunis.

Nchini Afrika Kusini,kiongozi wa chama cha EFF Julius Malema ametishia kuongoza maandamano makubwa zaidi yatakayoikwamisha nchi Jumatatu ijayo.

Soma pia:Kenya: Kufurika kwa wafanyibiashara kutoka China

Tayari wameifahamisha serikali kuwa hawataomba ridhaa ya kuandamana.

Na huko Senegal, kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko na wafuasi wake wanaandamana mjini Dakar kupinga azma ya rais aliyeko madarakani Macky Sall kuwania muhula wa tatu unaozua utata.

Kwa upande mwengine, uchunguzi unaendelea kuhusu kisa cha wizi wa vifaa vya uchaguzi uliotokea miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hayo yamebainika pale afisa mkuu mtendaji wa tume ya uchaguzi ya Kenya IEBC, Hussein Marjan alipojieleza mbele ya kamati ya bunge ya hesabu za umma.