Kenya kutuma wanajeshi kwa operesheni Turkana, Pokot Baringo
14 Februari 2023Hayo yametangazwa na serikali ikiwashutumu majambazi na wezi wa mifugo kwa kuwaua watu eneo hilo.
Kupitia taarifa, wizara ya ndani nchini Kenya ilisema siku ya Jumatatu kwamba katika muda wa miezi sita iliyopita, zaidi ya raia 100 wameuawa. Aidha polisi 16 wamepoteza maisha yao. Wanaoshutumiwa kufanya mauaji hayo ni majambazi na wezi wa mifugo katika maeneo ya kaskazini mwa Bonde la Ufa nchini Kenya.
Wizi wa mifugo, mizozano ya maeneo ya malisho kwa mifugo na vita vya kuwania vyanzo vya maji, ni matukio ya mara kwa mara miongoni mwa jamii katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya.
Kufuatia hali hiyo, serikali imetoa amri kwa raia wote wanaomiliki bunduki kinyume na sheria katika eneo hilo, kuzisalimisha mara moja ndani ya siku tatu zijazo.
Serikali ya nchi hiyo tayari imechapisha kwenye gazeti rasmi la serikali ya Februari 13, 2023, kwamba vikosi vya kijeshi vitapelekwa katika maeneo hayo kuanzia Februari 15, ili kusaidia vikosi vya polisi, kukabiliana na hali waliyoita kuwa dharura ya kiusalama, ambayo imesababishwa na ongezeko la visa vya ujambazi na wizi wa mifugo.
Rais William Ruto amesema: "Kuanzia kesho, tutakuwa na polisi pale, tutakuwa na wanajeshi pale, kwa hivyo tunataka kuwaambia watu wanaopenda amani, kama una bunduki ambayo hujapatiwa leseni na serikali, rudisha! Na wale wengine wote tunataka watoto wetu warudi shuleni, watu warudi shambani, kila mtu achunge ng'ombe yake."
Katika siku za hivi karibuni, magenge hayo yamezidisha kuwaua raia wasiokuwa na hatia, na hata maafisa wa usalama.
Wizara ya ndani imesema wakati wahalifu hao wanafanya hayo, pia wanateketeza moto shule, magari ya polisi na miundombinu mingine muhimu.
Wizara hiyo imeongeza kusema kuwa mamia ya watu wamelazimika kukimbia makwao.Hali bado ni tete Samburu, Kenya
Hata hivyo, hatua ya kuwapeleka wanajeshi katika maeneo ya ndani ya ndani ya nchi yanayokumbwa na machafuko, itahitaji kuidhinishwa na bunge.
Mnamo Septemba mwaka uliopita, watu wasiopungua 11 waliuawa katika Kaunti ya Turkana kaskazini mwa Kenya. Miongoni mwao walikuwa maafisa wanane wa polisi na chifu wa eneo lililovamiwa.
Mnamo Novemba mwaka 2012, zaidi ya maafisa wa polisi 40 waliuawa walipovamiwa ghafla.
Mauaji hayo mabaya ya idadi kubwa ya maafisa wa polisi yalifanyika eneo la Baragoi, kijiji cha mbali na chenye ukame kaskazini mwa Kenya, wakati polisi hao walipokuwa wakiwafuatilia wezi wa mifugo. Polisi waendelea na msako wa wezi wa mifugo nchini Kenya
Mnamo Agosti mwaka 2019, watu wasiopungua 12 wakiwemo watoto watatu waliuawa katika mashambulizi mawili tofauti yaliyofanywa na magenge yanayoiba mifugo kaskazini mwa Kenya.
Kenya, taifa linaloongoza kiuchumi miongoni mwa nchi katika kanda ya Afrika Mashariki, inakumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa miongo minne iliyopita, baada ya mvua kukosekana kwa misimu mitano. Hali hiyo imesababisha maafa makubwa ya mifugo na mimea kukauka mashambani, hususan maeneo ya kaskazini.
Chanzo: AFPE