Marsabit yaelezea wasiwasi kwa operesheni ya serikali Kenya
15 Februari 2023Siku mbili tu baada ya rais William Ruto kutangaza operesheni ya kijeshi katika eneo la bonde la ufa katika juhudi za kukusanya silaha haramu na kupambana na wezi wa mifugo katika eneo hilo,serikali ya kaunti ya Marsabit imeezelea masikitiko yake baada ya kuachwa nje ya orodha ya majimbo ambayo operesheni ya kijeshi inaendeshwa.
Kwa mujibu wa naibu gavana wa Marsabit Solomon Riwe,jimbo la Marsabit linalokaliwa na jamii za wafugaji kadhalika limekuwa likishambuliwa na majangili waliojihami kwa bunduki na kwamba jimbo hili lilipaswa kuangaziwa kwenye operesheni iliyotangawa na rais ili amani na usalama wa kudumu upatikane.
Kenya: Wakaazi Marsabit wakimbia makwao kwa kuhofia maisha
Akizungumza muda mfupi baada ya kutoa maoni yake kwenye jopo linaloangazia mageuzi kwenye idara ya polisi nchini,Riwe amedai kuwa operesheni hiyo kutoendeshwa Marsabit ni hatari kwa Maisha ya wakaazi wanaopakana na kaunti jirani ya Samburu kunakoendeshwa operesheni hiyo.
Wakaazi wanahofu huenda majangili wakakimbilia Marsabit
Baadhi ya wakaazi pia wanahofia kuwa,huenda majangili kutoka kaunti jirani kunakoendeshwa operesheni hiyo wakavuka na kuingia Marsabit hali inayoweza kuhatarisha Maisha ya raia.
Hata hivyo,kaimu kamishna wa Marsabit David Saruni ameshikilia kuwa,wizara ya usalama imeweka mikakati ya kukabiliana na majangili hao endapo watajaribu kuvuka na kuingia Marsabit wakikwepa mkono wa sheria.
Siku ya jumatatu,rais William Ruto alitangaza operesheni hiyo katika maeneo yaliyoripoti mashambulizi ya majangili wa mifugo japo alitoa muda wa siku tatu kwa raia kusalimisha silaha wanazomiliki kinyume cha sheria kabla ya operesheni hiyo kuanza rasmi.
Majimbo yaliyoorodheshwa kwenye operesheni hiyo ni Elgeyo Marakwet,Turkana,Pokot magharibi,Baringo,Laikipia na kaunti Jirani ya Samburu.
Michael Kwena DW Marsabit