1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa na Ujerumani kuteremka dimbani

5 Julai 2011

Timu za Ufaransa na Ujerumani ambazo zimefuzu tayari kiwango cha mtoano katika kundi A, zinachuana leo Jumanne 05.07.11 uwanjani Monchengladbach

https://p.dw.com/p/11omC
Marie-Laure Delie, na wenziwe wa timu ya taifa ya UfaransaPicha: dapd

Panatarajiwa kuwa na  patashika na nguo kiasi kuchanika, wakati wanawake wa timu hizo mbili za Ulaya, watakapoteremka uwanjani hii leo kuitafuta nafasi ya kwanza katika kundi hilo A.

Frauenfußball WM 2011 Deutschland vs Nigeria
Ni sherehe baada ya Simone Laudehr wa timu ya Ujerumani kuifunga NigeriaPicha: picture alliance/dpa

Kapteni wa timu ya taifa ya Ujerumani ya wanaume, Philip Lahm  ameiomba timu ya wanawake  ya Ujerumani kujizatiti kulishinda kwa mara nyengine taji la mashindano haya wakati wenyeji hao wanapoendelea kulitetea dhidi ya timu hiyo ya Ufaransa.

Timu ya wanawake ya Ujerumani  imefanikiwa kujishindia mara mbili mataji ya mashindano haya ya kombe la dunia, wanatazamia kukamilisha ushindi wa mara tatu  kama wenyeji  huku fainali zikitarajiwa kuchezwa  tarehe 17 mwezi huu mjini Frankfurt.

Baada ya kuifunga Canada  mabao 2-1 mjini Berlin, katika mechi rasmi ya ufunguzi wa mshindano haya mwaka huu, Ujerumani ilijizatiti lakini na mwishowe kutoka kwa ushindi wa bao moja pekee dhidi ya Nigeria wiki iliyopita,  na tayari ipo kwenye timu nane za mwisho. Hatahivyo leo inakabiliwa na kibarua kigumu inapoonana na Ufaransa na kuchukuwa uongozi katika kundi hilo A.

Kapteni Philip Lahm ambaye pia ni mchezaji nyota wa Bayern Munich, anamuomba kocha wa timu hiyo ya wanawake, Silvia Neid, kuchukuwa ushindi wa mashindano haya ambao waliukosa, timu hiyo ilipoanguka katika nafasi ya tatu baada ya kufungwa kwenye nusu fainali  na washindi Italia, mnamo mwaka 2006.

Lahm alisema mchezo mgumu kama ule wa timu hiyo ya wanawake dhidi ya Nigeria ulikuwa ni jambo la kawaida na sio jambo la kutia wasiwasi, akitoa mfano wa timu ya wanaume mnamo mwaka 2006, wakati anasema timu hiyo ilikuwa na matatizo yake lakini mwishowe ilifanikiwa kuishinda Poland 1-0. Amesema muhimu ni matokeo, na hivyo basi timu ya taifa ya Ujerumani haina budi  kushinda nusu fainlai ya mashindano haya.

Frauen-Fußball-WM 2011 Brasilien - Norwegen
Rosana , Cristiane, Marta, Maurine and Formiga wa timu ya BrazilPicha: picture-alliance/dpa

Brazil inajiunga na Ufaransa na Ujerumani katika robo fainali za mashindano haya  na ina pointi 6 mbele kutokana na michezo miwili na inashikilia uongozi katika kundi D, ikiwa na washindi wa mwaka 1995 wa kombe hilo la dunia, Norway,na Australia, ambao wote wana pointi 3 na watakutana katika mpambano wa mwisho wa kikundi na mshindi atajiunga na Brazil katika robo fainali hiyo.

Brazil inahitaji sasa pointi moja katika mechi yake ya mwisho dhidi ya timu Guinea ya ikweta  siku ya Jumatano ili kujihakikishia nafasi ya juu ambayo itaamua iwapo timu hiyo itacheza dhidi ya Marekani au Sweden.

Ama kwa upande wa timu ya pili ya Afrika, katika mashindano haya, Nigeria, pamoja na timu ya taifa ya Canada, zinatarajiwa kukamilisha kampeni zao kwenye mashindano ya mwaka huu  kwa kutafuta ushindi wa mwisho kila mmoja  hapo kesho  zitakapo onana katika mechi yao ya mwisho kwenye kundi A, kabla ya kurudi nyumbani.

Timu hizo zilizoshindwa na Ujerumani na Ufaransa zimeshindwa kujinyakulia pointi kila mmoja na zinatafuta ushindi huo kujimaarishia sifa na imani.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Afpe
Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed