Ujerumani kupambana na Ufaransa kwenye robo fainali
1 Julai 2011Timu ya taifa ya wanawake ya Ujerumani ilijizatiti dhidi ya upande wa Nigeria ambayo ilikuwa inang'ang'ana kusalia katika mashindano ya mwaka huu, lakini bahati ilionekana kuikwepa timu hiyo ya Afrika, wakati kunako dakika 54 za mchuano huo, mchezaji kiungo cha kati wa timu ya Ujerumani, Simone Laudehr alipoliona lango la Nigeria.
Hii ni baada ya awamu ya kwanza ya mechi hiyo kumalizika kwa timu zote kutoka sare ya 0-0 na baada ya hapo katika kipindi cha pili wachezaji hao wa Ujerumani walionekana kurudi uwanjani wakiwa na nguvu mpya.
Hatahivyo, baada ya ushindi wao dhidi ya Canada mnamo siku ya Jumapili, ushindi wa bao hilo moja haukuwa kama ulivyotarajiwa kwa timu hiyo bingwa mara mbili wa mashindano haya ya kombe la dunia ya wanawake.
Kocha wa timu hiyo Silvia Neid akizungumzia mechi hiyo alisema kuwa wamefanikiwa kuushinda mchezo wa jana (30.06.11), lakini wangeweza kucheza vizuri zaidi. walikuwa na wasiwasi mwingi, na tatizo ni kuwa walitaka kufuzu kwenye awamu inayofuata ya mchezo.
Kwengineko timu ya Ufaransa pia ilijinyakulia nafasi katika robo fainali za mashindano hayo baada nayo kuichabanga timu bingwa wa taji la CONCACAF, Canada, mabao 4-0, mjini Bochum.
Mabao mawili kutoka Gaetane Thiney, na mengine mawili yaliofungwa katika awamu ya pili ya mashindano hayo na Camille Abily na Elodie Thomis, yaliiipa timu hiyo ya Ufaransa pointi 6 za michezo miwili na imeichukuwa nafasi ya kwanza kwenye Kundi A ikifuatwa sasa katika nafasi ya pili na Ujerumani.
Ufaransa iliyoifunga Nigeria bao 1-0 katika mechi yao ya kwanza iliutawala uwanja dhidi ya Canada hapo jana, (30.06.11).
Sasa jukwaa limeandaliwa kwa mpambano unaosubiriwa kwa hamu kati ya timu hizo mbili za Uingereza, yaani Ujerumani na Ufaransa katika mechi ya mwisho ya kikundi mbele ya mashabiki 50,000 mjini Moenchengladbach siku ya Jumanne zote zikiwania nafasi ya kwanza katika kundi hilo A.
Changamoto sasa inaiangukia timu bingwa mara mbili wa mashindano haya ya wanawake, Ujerumani, baada ya ushindi wa mataji ya mwaka 2003 na 2007 mtawalia, na kikosi hicho cha Silvia Neid kinahitaji hekima zaidi iwapo kinatarajia kurudi uwanjani Frankfurt tarehe 17 mwezi huu Julai kushindana katika fainali.
Ama katika mechi za leo, (1.07.11), mashindano yanaendelea kwa kukutana kwa mara ya pili timu za kundi B, Japan dhidi ya Mexico mjini Leverkusen, na Uingereza ikionana na New Zealand mjini Dresden.
Mwandishi:Maryam Abdalla/Afpe