1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaifunga Canada

Halima Nyanza27 Juni 2011

Ujerumani jana ilianza vyema kuutetea ubingwa wake katika michuano ya Kombe la Dunia la Soka la wanawake mwaka 2011, iliyoanza jana hapa nchini, kwa kuifunga Canada mabao wawili kwa moja.

https://p.dw.com/p/11jwU
Mchezaji wa Ujerumani Celia Okoyino Da MbabiPicha: dapd

Kerstin Garefrekes ndiye aliyeanza kuliona lango la Canada, baada ya kuipatia timu yake bao la kwanza katika dakika ya 10.

Huku ikishangiliwa kwa nguvu na washabiki zaidi ya elfu 70, waliojitokeza katika uwanja wa Olympic mjini Berlin, akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, timu ya taifa ya Soka ya wanawake ya Ujerumani iliweza tena kujipatia goli lake la pili, baada ya Celia Okoyino da Mbabi kufanikiwa tena kutikisa nyavu za Canada.

Der offizielle WM-Ball Speedcell mit Logo
Picha: picture-alliance/dpa

Hadi ngwe ya kwanza ya mchezo huo kumalizika, Ujerumani ilitoka kifua mbele, lakini katika dakika ya 82, kipindi cha pili, Kapteni wa Timu ya soka ya Wanawake ya Canada Christine Sinclair aliweza kuipatia timu yake bao moja. Na kufanya matokeo ya mchezo huo kuwa mbili moja.

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika,  kocha wa Timu ya Soka ya Wanawake ya Ujerumani Silvia Neid, alielezea furaha yake baada ya ushindi huo katika mchezo wao wa kwanza.

Drei Eintrittskarten für das Eröffnungsspiel der FIFA Frauenfußball-Weltmeisterschaft 2011
Picha: picture-alliance/dpa

Na akizungumzia mchezo huo, alisema timu yake haikucheza vizuri katika kipindi cha kwanza lakini ilifanikiwa kupata mabao mawili na kwamba katika kipindi cha pili cha mchezo, timu ilijipanga vizuri zaidi lakini haikufanikiwa kupata magoli.

Kwa upande wake, Kerstin Garefrekes ambaye aliipatia Ujerumani bao la kwanza, alisema kutokana na kuwa ulikuwa mchezo wao wa kwanza walikuwa na wasiwasi kidogo, lakini amesema nafasi bado ipo ya wao kuweza kufanya vizuri zaidi.

Naye Kocha wa Canada Carolina Morace, akizungumzia mchezo huo alisema mechi ya kwanza katika kombe la dunia siku zote huwa ngumu. Hata hivyo amesema timu yake ilijitahidi.

Aidha katika matukio mengine yaliyojitokeza katika mechi hiyo, kapteni wa timu ya Canada, alivunjika pua, lakini alisisitizia kuendelea na mpira mpaka dakika ya mwisho na kuipatia timu yake bao.

Ushindi huo wa jana, umeifanya Ujerumani kuongoza katika kundi A, baada ya mchezo wa awali, Ufaransa kuibuka mshindi wa bao moja kwa bila dhidi ya wawakilishi wa  Afrika, Nigeria.

Katika dakika ya 56 ya mchezo huo, Marie-Laure Delie aliweza kuipa raha timu yake ya Ufaransa, baada ya kuikandamiza kwa bao moja Nigeria.

Awali akifungua michuano hiyo ya Kombe la Dunia la soka la Wanawake mwaka 2011, Rais wa Ujerumani, Christian Wulff alizitakia timu zote mechi zenye mafanikio.

Rais wa Ujerumani pia aliwakaribisha washabiki wa soka na kuzitakia timu zote 16 za wanawake kutoka duniani kote mchezo wa furaha na wa kiadilifu.

Aidha aliwashukuru waandaaji wote wa mashindani hayo kwa kujitayarisha miaka mingi kuifanya fainali hii kuwa ya aina yake. hususan Shirikisho zima la Soka la Ujerumani.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, afp)