1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia yatishia kuishitaki Libya

18 Mei 2011

Tunisia imetishia kuiripoti Libya kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa itayafyatua tena makombora katika eneo la Tunisia, baada ya mzozo wa Libya uliodumu kwa miezi mitatu sasa kuvuka hadi nje ya mipaka yake.

https://p.dw.com/p/11IzJ
Waasi wakielekeza mshambulizi yao kwa vikosi vya serikali
Waasi wakielekeza mshambulizi yao kwa vikosi vya serikaliPicha: dapd

Televisheni ya Taifa nchini Tunisia imesema serikali ya Tunisia itaitishia Libya kwa kuchukua hatua ya kidiplomasia kuhusiana na ongezeko la mashambulizi ya makombora ya vikosi vya serikali ya Libya kuelekea mipaka ya Tunisia.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Reuters, hapo jana maroketi manne yaliyotengenezwa Urusi yaliyofyatuliwa kutoka nchini Libya, yalianguka ndani ya ardhi yaTunisia.

Katika mji uliozingirwa wa Misrata, mapigano yalipamba moto baada ya kipindi cha utulivu, huku daktari mmoja akisema kuwa watu saba wamejeruhiwa wengi wao wakiwa ni wapiganaji wa waasi katika mapambano ya hapo jana dhidi ya vikosi vya serikali.

Wakati huo huo, waasi wa Libya na duru za kiusalama nchini Tunisia wamesema kuwa Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Mafuta nchini Libya (NOC) alijiondoa serikalini na kukimbia Tunisia, tukio ambalo ikiwa litathibitishwa litakuwa ni pigo kubwa kwa juhudi za Muammar Gaddafi kung'ang'ania madaraka.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Mohammed Khelef