Ndege za NATO zalenga mji mkuu wa Libya
14 Mei 2011Hiyo jana, NATO ilituhumiwa na serikali ya Muammar Gaddafi mjini Tripoli, kuwa imesababisha vifo vya viongozi 11 wa kidini wa Kiislamu katika shambulio la anga lililolenga mji wa mafuta Brega. Mji huo unadhibitiwa na vikosi vya Gaddafi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Franco Frattini amesema, Gaddafi amejeruhiwa katika shambulio jipya lililoilenga nyumba yake na kiongozi huyo huenda hayupo tena mjini Tripoli. Wakati huo huo, televisheni ya taifa ya Libya imetangaza kanda, yenye sauti ya Gaddafi, akisema kuwa yeye ni mzima na yupo mahala ambapo NATO haitoweza kumpata.
Wakimbizi wamiminika Italia
Wakati huo huo, wakimbizi wanaendelea kumiminika kusini mwa Italia wakitokea Libya. Kwa mujibu wa walinzi wa pwani wa Italia, takriban wakimbizi 1200 wamewasili kwa boti katika kisiwa cha Lampedusa kilicho katika Bahari ya Mediterania. Takriban wahamiaji hao wote, ni watu waliokimbia Libya hata kabla ya mapigano kutokea nchini humo. Ripoti zinasema kuwa boti zingine zimeonekana baharani zikiwa na wakimbizi.
Inatathminiwa kuwa hadi wakimbizi 11,000 wametua kisiwani Lampedusa, tangu mapambano kuzuka kati ya kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi na waasi wa Libya wanaoungwa mkono na jumuiya ya kujihami ya NATO. Kisiwa cha Lampedusa kina ukubwa wa kilomita 20 za mraba na ni kiasi ya kilomita 130 tu kutoka Tunisia.