Waasi wa Libya ziarani Marekani
14 Mei 2011Marekani hata hivyo, haikulipa kundi hilo hadhi ya kulitambua kidiplomasia baada ya mkutano na waasi hao wa NTC katika Ikulu ya Marekani jana. Waasi hao, wakiongozwa na kiongozi wao Mahmud Jibril wako mjini Washington Marekani kushinikiza kutambuliwa rasmi na kupata misaada zaidi ya kifedha.
Wakati huohuo, televisheni ya taifa ya Libya ilirusha taarifa anayoripotiwa kuwa ni ya kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi, ambaye alikuwa akilaani shambulio la Alhamisi lililofanywa na majeshi ya NATO katika makaazi yake. Licha ya ripoti zilizotolewa awali kwamba kiongozi huyo wa Libya amejeruhiwa katika shambulio hilo, amesema katika taarifa yake kwamba hakudhurika na yuko katika sehemu ambapo mabomu ya majeshi ya NATO hayawezi kumfikia. Msemaji wa Gaddafi amesema kiongozi huyo bado yuko katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.