Sudan: Waziri mkuu Abdalla Hamdok ajiuzulu
2 Januari 2022Waziri mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok alipokuwa akitangaza hatua hiyo kupitia televisheni, alisema anaachia wadhifa huo, ili kuruhusu mtu mwingine kusaidia taifa hilo kuvuka katika kipindi cha mpito cha mabadilishano ya kidemokrasia ya madaraka.
Soma Zaidi: Kumrejesha Hamdok madarakani kunamaanisha nini?
Aidha, ametoa mwito wa kufanyika kwa majadiliano ili kufikiwa kwa makubaliano mapya kuhusiana na namna serikali hiyo mpya itakavyofikiwa.
Sudan inapita katika kipindi kigumu kinachotishia mustakabali wa taifa hilo, na kulingana na Hamdok juhudi zake za kuliepusha taifa hilo lisitumbukie kwenye janga zaidi hazikufua dafu.
Kuondoka kwa Hamdok kunaonekana kama pigo kubwa na huenda taifa hilo likaingia kwenye mzozo mkubwa zaidi, ikiwa ni miaka mitatu baada ya vuguvugu lilimuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo Omar al-Bashir.
Hamdok hatimaye alichaguliwa kuwa waziri mkuu katika sehemu ya makubaliano na jeshi. Lakini hata hivyo jeshi hilo lilifanya mapinduzi Oktoba 25 mwaka jana yaliyoipindua serikali ya Hamdok, lakini baada ya vuta nikuvute, waziri mkuu huyo alirejea kuongoza serikali, mwezi Novemba.
Lakini licha ya makubaliano na jeshi, kuliendelea kushuhudiwa maandamano nchini humo ya kudai kurejeshwa kwa serikali ya kiraia. Vikosi vya usalama vilitumia nguvu kubwa kuwatawanya waandamanaji hao, hatua iliyosababisha vifo vya baadhi ya waandamanaji.
Soma Zaidi: Sudan: Vikosi vya usalama vyatumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji
Mashirika: DW