Kumrejesha Hamdok madarakani kunamaanisha nini?
23 Novemba 2021Mnamo siku ya Jumapili, jeshi lilikubaliana na Abdalla Hamdok kumrejesha madarakani kama mkuu wa baraza jipya la mawaziri ambao wengi ni wasomi na wataalam kuelekea uchaguzi.
Lakini makubaliano hayo yamewaghadhabisha wanaharakati wa demokrasia wanaomtuhumu Hamdok kwa kuruhusu kutumiwa kama kifumba macho chini ya muendelezo wa utawala wa kijeshi.
Sehemu kubwa ya jumuiya ya kimataifa imeyashutumu mapinduzi hayo na kutaka kurejeshwa angalau kwa utawala wa kiraia.
Marekani ilisitisha misaada yake kwa taifa hilo linalokabiliwa na umaskini wa fedha, wakati likijaribu kujiinua polepole baada ya miongo mingi ya kutengwa chini ya aliyekuwa rais wa zamani Omar al-Bashir aliyeng'olewa madarakani kufuatia maandamano makubwa mnamo mwaka 2019.
Vuguvugu la Uhuru na Mabadiliko ambalo huleta pamoja vyama vya kisiasa nchini humo na wanaharakati, tayari limeyapinga makubaliano hayo likisema limejitolea kuhakikisha utawala wa kijeshi unatokomezwa.
Lakini jeshi linawasiwasi kurejesha utawala kwa raia kwani itawaweka wakuu wake katika hatari ya kushtakiwa kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu au itawafanya wakuu wake kukosa ushawishi na udhibiti kwenye sekta muhimu za uchumi.
Je ni kwa nini jeshi lilikubali kumrejesha waziri mkuu? Bila shaka jeshi lilihitaji kufanya jambo.
Mkuu wa majeshi Jenerali Abdel-Fattah Burhan amekumbwa na shutma na shinikizotele tangu alipochukua madaraka kamili Oktoba 25. Bila shaka jeshi lilihitaji kufanya jambo.
Hivyo basi, majenerali wa kijeshi wamemrudisha Hamdok madarakani kama hatua ya kuleta utulivu nchini kuelekea uchaguzi ambao umepangwa kufanyika Julai mwaka 2023 na tayari jumuiya ya kimataifa imeunga mkono hatua hiyo.
Wamefanya hivyo pia kwa sababu ya maandamano makubwa ambayo yameanza kushuhudiwa mithili ya yale yaliyoumaliza utawala wa Omar al-Bashir, ambapo tayari wanajeshi wanadaiwa kuwaua waandamanaji 40.
Lakini je, hatua ya kumkabidhi Hamdok madaraka inaondoa mapinduzi yaliyofanywa? Bila shaka jibu ni la hasha.
Jeshi linaendelea kuwa na udhibiti mkubwa na kwa kubuni baraza la mawaziri ambao ni wasomi na wataalam, makubaliano hayo yanawaweka pembeni wanaharakati wa vuguvugu la mageuzi na vilevile vyama vya kisiasa.
Jihad Mashamoun ambaye ni mtafiti wa Sudan na pia mchambuzi wa kisiasa amesema haamini ikiwa serikali ya Hamdok itafanya kazi vyema kwa sababu haitambuliwi na waandamanaji.
Chama cha wataalam wa Sudan ambacho kiliongoza maandamano dhidi ya Omar al.-Bashir kimelaani makubaliano hayo na kusema ni sawa na jaribio la kuhalalisha mapinduzi.
Jeshi limesema hawatarudi katika mpango wa kugawana madaraka tena serikalini kama ilivyokuwa kabla ya Oktoba 25 likisema lilijaa mivutano ya ndani kwa ndani.
Nafisa Hajar, wakili kuhusu masuala ya haki za binadamu ambaye pia ni naibu mkuu wa chama cha mawakili mjini Darfur anasema maadamu makubaliano hayo yalifanywa chini ya usimamizi wa jeshi na yalienda kinyume na matakwa ya vuguvugu la waandamanaji, anaamini matumizi ya nguvu ya majenerali wa kijeshi dhidi ya waandamanaji, yalimuacha Hamdok bila chaguo.
Swali jingine ni je, kuna matumaini ya sudan kurejea katika utawala wa kidemokrasia?
Kunaonekana kuwa na njia mbili kufikia demokrasia lakini zote zina changamoto.
Hamdok anaweza kushirikiana na majenerali wa kijeshi ili kusafisha njia ya uchaguzi, hatua itakayoinua hadhi yake na pia uungwaji wa kimataifa kurejesha juhudi za mpito wa kisiasa. Lakini huenda hiyo itamaanisha kurudi tena kwenye mvutano kati ya pande hizo mbili katika miaka miwili ijayo.
Njia nyingine ni hatua hiyo ya waandamanaji kuapa kuendeleza maandamano hadi jeshi liachie madaraka kwa raia. Hatua hii itamaanisha wanajeshi ndio watapoteza, lakini mkwamo kati yao unaweza kutanua machafuko zaidi nchini.
"Katika hali hiyo demokrasia inaweza kutimia ila itaacha nchi ikiwa imegawika zaidi," amesema Alex Waal, mtaalamu wa masuala ya Sudan katika chuo kikuu cha Tufts nchini Marekani.
(APE)