1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi Sudan yaendelea

1 Novemba 2021

Waandamanaji wanaopinga mapinduzi Sudan wameweka vizuizi barabarani mjini Khartoum siku moja baada ya kamatakamata ya waandamanaji wakati maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi yakiingia siku ya nane.

https://p.dw.com/p/42QX9
Sudan | Pro Demokratie Proteste in Khartoum
Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Watu watatu waliuwawa kwa kupigwa risasi huku wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa katika maandamano ya siku ya Jumamosi, hii ikiwa ni kulingana na taarifa za maafisa wa afya, walioripoti kuwa waliouwawa walikuwa na majeraha ya risasi kichwani, vifuani na tumboni.

Hata hivyo maafisa wa polisi wamekanusha ripoti hizo na kusema hakuna risasi za moto zilizotumika kuwatawanya waandamanaji.

"Tunasema hapana kwa utawala wa kijeshi" walisema waandamanaji waliokuwa wamebeba bendera za Sudan mjini Khartoum na miji mingine huku maafisa wa usalama wakiwarushia gesi za kutoa machozi ili kuwatawanya.

Soma zaidi:Upinzani kwa jeshi la Sudan wazidi

Maelfu ya waandamanaji wameendelea kujitokeza kupinga mapinduzi ya kijeshi yaliofanyika Oktoba 25 wakati mkuu wa jeshi hilo jenerali Abdel Fattah al-Burhan alipoivunja serikali, kutangaza hali ya dharura na kuwakamata viongozi wa kiraia.

Hatua hiyo ilikosolewa vikali kimataifa, misaada muhimu ikisitishwa na viongozi wa mataifa yalio na nguvu duniani wakitaka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia pamoja na kulitaka jeshi kuacha kuwaandama waandamanaji.

Marekani yasema mapinduzi yanarejesha nyuma maendeleo ya Sudan

Italien I G20 Summit I Joe Biden
Rais wa Marekani Joe Biden Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden ameyafananisha mapinduzi yaliyofanywa na Burhan kama njia moja ya kurejesha nyuma maendelea ya Sudan huku Umoja wa Afrika ukifuta kwa muda uwanachama wa Sudan katika Umoja huo kwa kuchukua madaraka kinyume cha katiba.

Benki ya dunia na Marekani zimezuwiya msaada kwa taifa hilo hatua inayotazamiwa kuathiri pakubwa uchumi wake ambao tayari unayumba.

Huku hayo yakiarifiwa Hapo jana televisheni ya taifa imeripoti kuwa Burhan amemfuta kati mwendesha mashitaka mkuu kufuatia kuachiliwa huru kwa viongozi kadhaa waliofungamanishwa na utawala uliopinduliwa wa rais wa zamani Omarl al Bashir.

Wakati uo huo Volker Perthes, muakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan amesema hapo jana alikutana na Waziri Mkuu Abdallah Hamdok ambaye yuko chini ya ulinzi mkali wa kijeshi nyumbani kwake na kwamba anaendelea vizuri na wamezungumza kwa kina kuhusu uwezekano wa kuwa na mpatanishi na kile kitakachofuata baadae nchini Sudan.

Tangu Agosti mwaka 2019 Sudan imeongozwa na Barazala la pamoja lililowajumuisha viongozi wa kijeshi na wale wa kiraia kama sehemu ya hatua iliyocheleweshwa sasa ya kuikabidhi nchi katika utawala wa kiraia.

Baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi Burhan ameahidi kuwa serikali mpya ya kiraia itaundwa hivi karibuni. Abdel Fattah al Burhan anaendelea kusisitiza kuwa kilichofanyika sio mapinduzi bali ni kurekebisha serikali ya mpito ya Sudan.

Chanzo: reuters/afp