1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Sudan kupinga utawala wa kijeshi

20 Desemba 2021

Maelfu ya watu wameandamana hadi Ikulu ya Rais katika mji mkuu wa Khartoum wakipinga mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25 na kushinikiza kutohusika tena kwa jeshi katika kipindi cha mpito kuelekea kwa demokrasia kamili.

https://p.dw.com/p/44YFV
Sudan, Khartoum | Proteste gegen den Militärputsch
Picha: AFP/Getty Images

Hata hivyo waandamanaji hao walikabiliwa na mabomu ya kutoa machozi kutoka kwa vikosi vya usalama.

Ilikuwa ni hali ya mguu niponye kwa waandamanaji nchini Sudan waliomiminika barabarani kupinga utawala wa kijeshi.

Madaktari wamesema idadi kubwa ya watu wamejeruhiwa katika maandamano hayo, lakini licha ya juhudi za vikosi vya usalama kujaribu kuwatawanya waandamanaji hao, baadhi walifanikiwa kufika kwenya lango la Ikulu.

Soma zaidi: Hamdok arudishwa tena madarakani Sudan

Waandamanaji wamewahimiza watu zaidi kujiunga kwenye maandamano hayo huku video kutoka eneo la tukio zikionyesha waandamanaji waliosalia wakirushiwa mabomu ya kutoa machozi.

Maandamano hayo, ambayo ni ya tisa na mojawapo ya maandamano makubwa kuwahi kufanyika tangu kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi, yamefanana na yale ya mnamo mwaka 2018 yaliyopelekea kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir.

Maandamano yameshadidi licha ya kurejeshwa madarakani waziri mkuu Abdalla Hamdo

Sudan, Khartoum | Proteste gegen den Militärputsch
Waandamanaji wakielekea Ikulu ya Rais mjini KhartoumPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi yameshadidi hata baada ya kurejeshwa madarakani waziri mkuu Abdalla Hamdok mwezi uliopita, wakati waandamanaji wakishinikiza kutohusika tena kwa jeshi katika kipindi cha mpito kuelekea kwa uchaguzi huru.

Kwa ujasiri mkubwa, waandamanaji walimimika kwenye barabara kuu inayoelekea Ikulu ya Rais na kuimba "Watu wana nguvu na kamwe haturudi nyuma," wakati wengine wakikwepa mitungi ya mabomu ya kutoa machozi.

Muhammad Omar, ni mmoja wa waandamanaji. "Niko hapa kwa sababu ninapinga kabisa mkabata huu wa kisiasa kwani hauwakilishi matakwa ya wananchi"

Kwa mujibu wa wizara ya afya nchini humo, watu wapatao 123 wamejeruhiwa katika patashika hiyo kwenye mji mkuu wa Khartoum, pamoja na miji yake pacha ya Bahri na Omdurman na mji wa mashariki wa Kassala. Kadhalika, kamati kuu ya madaktari wa Sudan imesema watu 45 wameuawa tangu mapinduzi ya kijeshi mnamo Oktoba 25.

Soma pia: Mahakama Sudan yaamuru huduma za Intaneti kurejeshwa

Madaktari wanaohusishwa na vuguvugu la maandamano wamevishtumu vikosi vya usalama kwa kutumia risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji, kuwashambulia na kuwaibia. Vikosi vya usalama pia vinashtumiwa kwa kuzingira hospitali na kurusha mabomu ya machozi kwenye milango ya hospitali.

Hata hivyo hakukuwa na taarifa yoyote kutoka kwa polisi juu ya matukio hayo.

Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha maandamano yakifanyika pia katika miji mengine ikiwemo Port Sudan, El-Deain, Madani na Kassala.

Mnamo siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu Abdalla Hamdok kupitia taarifa alitahadharisha kuwa mapinduzi ya Sudan yanakabiliwa na kikwazo na kwamba misuguano ya kisiasa kutoka pande zote kunatishia umoja na utulivu nchini humo.