1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia: Umoja wa Mataifa kuongeza vikosi vya walinda amani

Admin.WagnerD21 Oktoba 2010

Umoja wa Mataifa unakusudia kuongeza wanajeshi wa kulinda amani nchini Somalia, lakini Somalia kwenyewe kuna mgogoro wa Bunge kuhusiana na uteuzi wa Waziri Mkuu mpya, Mohamed Abdullahi Mohammed

https://p.dw.com/p/Pjqs
Mmoja wa wanajeshi wa Ujerumani kwenye vikosi vya kimaitaifa
Mmoja wa wanajeshi wa Ujerumani kwenye vikosi vya kimaitaifaPicha: Daniel Scheschkewitz

Jambo moja liko wazi: Somalia inahitaji msaada wa hali na mali, kisiasa na kiusalama, kuikwamua kwenye miongo miwili ya maangamizi. Huo ndio ujumbe unaoungwa mkono na Umoja wa Afrika na Marekani katika mpango wa kuongeza wanajeshi wa kulinda amani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iliyozongwa na machafuko. Lakini kisicho wazi ni namna gani msaada huo utafanikisha azma inayolengwa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika, Johnnie Carson, alisema hapo jana (20 Oktoba 2010) jijini Washington kwamba, nchi yake inaunga mkono kimsingi kuongeza wanajeshi wa kulinda amani, ingawa hakusema ni kwa idadi gani.

Tayari Rais Yoweri Museveni wa Uganda, alishasema nchi yake iko tayari kupeleka wanajeshi wote 20,000 wanaohitajika kwenye opereshini hii, ikiwa watagharamiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, miaka mitatu ya kuwepo kwa walinda amani wa AMISOM kwenye nchi hiyo, bado haijaleta usalama kwa Wasomali wenyewe. Bado wanamgambo wa Al Shabbab ndio wanaoshikilia sehemu kubwa ya Somalia na bado serikali ya mpito ya nchi hiyo haijakuwa na uimara wa kutosha kuweza kutawala.

Vikosi vya serikali vikijitayarisha kupambana na wapiganaji wa Al Shabbab
Vikosi vya serikali vikijitayarisha kupambana na wapiganaji wa Al ShabbabPicha: AP

Jitihada za serikali kujiimarisha ili hatimaye iwe na uwezo wa kudhibiti hali, zimekuwa zikikwamishwa na misuguano ya ndani kwa ndani. Mwezi uliopita aliyekuwa Waziri Mkuu, Omar Abdirashid Ali Shemarke alilazimika kujuzulu, kutokana na kushindwa kufanya kazi na Rais wake, Sheikh Sharif Ahmed.

Na jana waziri mkuu mpya aliyeteuliwa na Rais Ahmed, Mohamed Abdullahi Mohamed alishindwa kupigiwa kura ya kumpitishwa Bungeni, baada ya wabunge kugombana juu ya njia ya kupiga kura hiyo. Kura hiyo imeahirishwa hadi Jumamosi ijayo.

Mohamed Abdullahi ni mwanadiplomasia aliyesomea nchini Marekani, na mwenyewe anajinasibisha na siasa za kutokufungamana na kundi lolote miongoni mwa makundi yanayogombana nchini mwake. Mapema aliwaambia wabunge hao kwamba hamu yake ni kuiona Somalia inajikwamua kutoka dimwbi la machafuko.

"Mimi si mtu wa kundi lolote, la kidini au la kisiasa, ama kundi lolote lile zaidi ya kuwa mimi ni Msomali ambaye anataka kushiriki kwenye ujenzi wa taifa ambalo limekuwa halina serikali yenye ufanisi kwa karibuni miongo miwili sasa." Alisema Mohammed Abdullahi.

Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba, kuahirishwa kwa kura hii ni mbinu tu ya Spika Sharif Hassan Sheikh Aden, ambaye ana mgogoro wake na Rais Ahmed. Kwa kawaida spika ndiye anayekaimu nafasi ya urais, wakati rais anapokuwa na dharura.

Serikali hii inayoungwa mkono na madola ya Kimagharibi inalindwa na vikosi vya Umoja wa Afrika mjini Mogadishu, lakini makundi ya Kiislam yanadhibiti eneo kubwa la mji mkuu huo na maeneo ya kati na kusini ya Somalia. Kuwepo kwa wanajeshi wa kigeni katika ardhi ya Somalia, kunatajwa na wachambuzi kwamba kunawapa sababu wapiganaji hao wa Kiislam kutumia bango la uzalendo katika mapambano yao na hivyo kupata uungwaji mkono kirahisi kutoka kwa vijana na Wasomali wanaoishi nje.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters

Mhariri: Josephat Charo