1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Somalia amteua Mmarekani mwenye asili ya Kisomali kuwa waziri mkuu mpya

15 Oktoba 2010

Mohammed Abdulahi anakabiliwa na kibarua kipevu cha kuiongoza serikali ya mpito inayoyumba, inayokabiliwa na mizozo ya ndani ya kisiasa na rushwa

https://p.dw.com/p/Pf6g
Rais wa serikali ya mpito ya Somalia, Sheik Sharif Sheik AhmedPicha: AP

Rais wa Somalia, Sheikh Sharif Ahmed, amemteua Mmarekani mwenye asili ya Kisomali kuwa waziri mkuu mpya wa Somalia. Uteuzi wa Mohammed Abdullahi, mwanadiplomasia wa zamani aliyesomea nchini Marekani, ni juhudi mpya ya kuimarisha mchakato wa kukabiliana na wanamgambo wanaolidhibiti eneo kubwa la Somalia.

Mohammed Abdullahi Mohamed mwenye umri wa miaka 49, aliyeteuliwa jana (14.10.2010) atachukua nafasi iliyoachwa na waziri mkuu wa zamani, Omar Abdirashid Shamarke, aliyejiuzulu mwezi uliopita, kufuatia hatua ya serikali kushindwa kuzima upinzani wa wanamgambo ambao umesababisha vifo vya maelfu ya Wasomali tangu mwanzoni mwa mwaka 2007.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Mohammed Abdullahi Mohamed, amesema, "Jambo la kwanza nitakalolipa kipaumbele kikubwa ni usalama na kutimiza majukumu yangu kwa umma wa Somalia. Tunahitaji kupambana na wanamgambo wanaosababisha umwagikaji mkubwa wa damu usiokuwa na maana, kwa kupigana nao au kwa kufanya nao maridhiano, kama watakuwa tayari kufanya hivyo,"

Ofisi ya rais wa Somalia imesema katika taarifa yake kwamba Abdulahi ni msomi aliyejishughulisha zaidi na masuala ya utawala, usimamizi wa miradi na kutanzua mizozo na anatarajiwa kuunda baraza jipya la mawaziri katika kipindi cha mwezi mmoja. Uteuzi wake utahitaji kuidhinishwa na bunge la Somalia, ingawa wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema itakuwa hatua ya kawaida ya kuufanya uteuzi wake kuwa rasmi, kwani rais aliwashauri wabunge kabla kumteua.

Abdulahi anakabiliwa na kibarua kipevu cha kuiongoza serikali ya mpito inayoyumba, inayokabiliwa na mizozo ya ndani ya kisiasa, rushwa na iliyobanwa na wanamgambo katika sehemu ndogo ya mji mkuu Mogadishu.

Abdulahi ana nafasi kubwa ya kufanikiwa

Afyare Abdi Elmi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa chuo kikuu cha Qatar amesema ana matumaini kwa kuwa Abdulahi anatokea nje ya Somalia, na umri wake ni mdogo, huenda akasaidia kuipiga jeki serikali kwa kutoa mawazo mapya na muelekeo tofauti. Amesema anatumai pia kuwa ataunda baraza dogo la mawaziri wachapa kazi, na nafasi nzuri ya kufaulu.

Hassan Mohamed, kiongozi wa koo moja nchini Somalia amesema ana hakika kwamba waziri mkuu mteule ataiimarisha serikali ya mpito ya nchi hiyo. Amesema kwa kuwa anatokea kusini mwa Somalia, kutamsaidia kuwashawishi wanamgambo wa kundi la al Shabaab kuiunga mkono serikali ya mpito na hata kujiunga na serikali hiyo.

Utekaji nyara

Kwingineko nchini Somalia watu waliokuwa na bunduki waliokuwa wamejifunika nyuso zao wamewateka nyara wafanyakazi wawili wa shirika la misaada la Save the Children, raia wa Uingereza na Msomali, katika uwanja wa shirika hilo mjini Adado karibu na mpaka na Ethiopia. Mkaazi wa eneo hilo, Mpalim Bashir amesema hakujua ni nani aliyewateka nyara wanaume hao wawili hapo jana jioni na kuongeza kuwa hali ya wasiwasi mjini Adado imeongezeka huku makundi ya wanamgambo yakiongeza wapiganaji wao kusini mwa Somalia na huenda wakajaribu kuteka mji huo kutoka mikononi mwa wale wajaoudhibiti kwa sasa.

Katika taarifa yake shirika la Save the Children limesema kwa wakati huu halina maelezo zaidi kuwahusu wafanyakazi wake waliotekwa nyara wala hali yao ya afya. Wizara ya mambo ya nchi za kigeni ya Uingereza imesema inachunguza ripoti za kutekwa nyara Muingereza huyo nchini Somalia.

Wakati huo huo wanamgambo wa Kisomali pia wamemteka nyara afisa wa ulinzi wa shirika moja la misaada, raia wa Zimbabwe pamoja na mpambe wake kutoka nyumbani kwao katika eneo la Adado. Walioshuhudia tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo wanasema wawili hao walitekwa nyara na washambuliaji waliokuwa wamejihami na silaha nzito na maguruneti, lakini hawajui walikopelekwa watu hao.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman