Papa Francis aizuru Hungary, ahimiza amani na kuvumiliana
28 Aprili 2023Hotuba hiyo ya kwanza ya Papa Francis katika ziara yake ya siku tatu nchini Hungary, imetolewa mbele ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Viktor Orban na viongozi wengine wa ngazi za juu nchini Hungary.
Soma zaidi: Papa Francis kuanza ziara nchini Hungary
Papa Francis amesema Ulaya inapaswa kurejea katika mitazamo ya waasisi wake, ya kujenga diplomasia yenye uwezo wa kuunganisha watu, badala ya kupanua migawanyiko. Ameonya dhidi mwamko wa kivita kuzidi nguvu ukomavu uliofikiwa baada ya madhila ya vita, na kuruhusu hatua za kurudi nyuma katika hali ambayo ni mithili ya ugomvi wa kitoto.
Akemea kauli za kuchochea vita
''Ni kama vile tunashuhudia kutoweka kwa ndoto ya amani, na nafasi yake ikichukuliwa na wanaopiga ngoma ya vita,'' amesema kiongozi huyo wa kidini, na kuongeza kuwa azma ya kujenga amani na utengamano wa jumuiya ya kimataifa inayumba, kanda za ushawishi zinaundwa, tofauti zinatiliwa mkazo, utaifa unaimarika na lugha kali ya makabiliano inapaza sauti.
''Kwenye ngazi ya kimataifa, inaonekana kama siasa zinasaidia kuchochea hisia badala ya kutafuta suluhisho,'' amesikitika Papa Francis.
Soma zaidi: Papa Francis ahimiza mazungumzo kumaliza mzozo wa Sudan
Papa Francis na Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban wana maoni sawa katika kuhimiza mazungumzo kama juhudi ya kumaliza vita vya Ukraine, lakini wanatofautiana juu ya suala la wahamiaji.
Orban ni mfuasi wa sera kali ya kuwapinga wahamiaji kama njia ya kulinda Ukristo ndani ya Ulaya, wakati Papa Francis akitaka wale wanaokimbia vita na umasikini wakaribishwe.
Wafungulieni milango wanaokimbia vita na umasikini
Katika hotuba yake Papa Francis amesisitiza haja ya kuwafungulia milango wengine, na kuonya dhidi ya jamii kujifungia ndani ya mipaka yake.
Amesema Ulaya inapaswa kutafuta njia za kisheria za mchakato wa kukabiliana na changamoto lukuki zisizoepukika, ili kuandaa mustakabali ambao kama sio wa pamoja, hauwezi kuwepo.
Soma zaidi: Hungary ilivunja sheria kuwazuia wahamiaji
Papa alionekana mchangamfu licha ya matatizo ya goti yanayomfanya atembee katika kiti cha magurudumu. Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu afya yake akiwa njia kwenda Hungary, mkuu huyo wa kanisa Katoliki amejibu kwa utani kuwa angali hai, kwa sababu ''gugu sugu haling'oleki.''
Ziara yake rasmi nchini Hungary ni kutimiza ahadi aliyoiweka mwaka 2021 kwa waumini katika taifa hilo la Ulaya ya kati, baada ya kusalia katika mji mkuu wa nchi hiyo Budapest kwa muda wa masaa saba tu akifunga kongamano la kikanisa.
-Vyanzo: afpe, rtre, ape