Hungary ilivunja sheria kuwazuia wahamiaji
17 Desemba 2020Mahakama ya Juu ya Umoja wa Ulaya imetoa uamuzi leo Alhamisi kwamba Hungary imevunja sheria kwa kuwazuia wahamiaji wanaoingia nchini humo haki ya kutafuta hifadhi na badala yake kuwazuia kwenye kambi za muda zilizopo katika mpaka wake na Serbia.
Mahakama ya Umoja wa Ulaya katika uamuzi wake imesema Hungary imeshindwa kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha upatikanaji mzuri wa utaratibu wa kutoa ulinzi wa kimataifa "kwa wahamiaji wanaoingia kutoka Serbia na kuwaacha bila uwezekano wa kuwasilisha maombi ya hifadhi.
Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, iliwasilisha kesi dhidi ya Hungary kutokana na sheria iliyoanzishwa mnamo 2015, wakati zaidi ya wahamiaji milioni 1 walipoingia Ulaya, wengi wao wakiwa wakimbizi kutoka Syria au Iraq, kuwasili Ugiriki kwa nia ya kutafuta hifadhi nchini Ujerumani au kwenye nchi za Scandinavia.
Maelfu ya wahamiaji walipitia mataifa ya eneo la Balkan, huku serikali ya Hungary inayopinga wahamiaji ikiweka uzio wa nyaya za wembe ili kuwazuia kuingia nchini humo na kupanua matumizi ya kile walichokitaja kama "hali ya shida inasababishwa na uhamiaji wa watu wengi" ambayo kisheria inawarusu kuanzisha maeneo mawili ya ''eneo linalozunguka bandari ya kuingia katika nchi'' ambapo wahamiaji wanazuiliwa.
Waziri mkuu Viktor Orban azidi kuhimiza kuhusu ulinzi wa mipaka.
Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imesisistiza kuwa watu wanaoingia Hungary walipelekwa kwa lazima katika kambi hizo za muda, na kuwanyima haki yao ya kuomba ulinzi wa kimataifa.
Katika uamuzi wake, Mahakama ya Juu ya Umoja wa Ulaya yenye makao yake Luxemburg ilisema kuwa haki ya watu kuomba hifadhi "ni hatua muhimu" katika kutoa ulinzi kwa wale wanaotafuta hifadhi kutokana na vitisho dhidi ya maisha yao au usalama wao na kwamba nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya hazipaswi kuichelewesha bila ya sababu za msingi.
Mahakama hiyo imesema nchi wanachama lazima zihakikishe kwamba wahamiaji wanaweza kutuma maombi ya kutaka hifadhi hata wakiwa kwenye mipaka, mara tu wanapotaka kufanya hivyo.
Pia mahakama hiyo imesema uamuzi wa Hungary kuwazuilia wakimbizi wengine ndani ya kambi za muda ambazo kwa sasa zimevunjwa, wakati maombi waliyowasilisha awali kutaka hifadhi yamezingatiwa inaashiria kuwaweka "kizuizini" wahamiaji.
Hungary imekuwa na maoni makali juu ya uhamiaji huku Waziri Mkuu Viktor Orban akihimiza taifa hilo kudhibiti mipaka. Na mara nyingi amekuwa akisema kuwa ni muhimu kuzuia wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati na Afrika kuingia Hungary kwa lengo la kuhifadhi dini ya Kikristo ya tamaduni ya taifa hilo.
Mwandishi: Saumu Njama
Mhariri: Grace Patricia Kabogo