Merkel amshutumu waziri mkuu Orban wa Hungary
5 Julai 2018Kansela pia atakutana na viongozi wa vyama vitatu ambavyo vinaunda muungano wa serikali leo kwa mazungumzo mazito kuhusiana na mswada wa makubaliano ya uhamiaji yaliyofikiwa wiki hii pamoja na waziri wake muasi wa mambo ya ndani Horst Seehofer.
Katika mpambano dhahiri kuhusiana na maadili ya ulaya katika wakati ambapo uhamiaji unatishia umoja katika mataifa hayo ya Ulaya , Merkel na Orban kila mmoja akijionesha kuwa mtetezi mkubwa wa lengo la kundi hilo la mataifa. "Tatizo kama ninavyoliona, na pale tofauti ilipo, ni kwamba ni lazima tukumbuke kwamba tunazungumza juu ya binadamu", Merkel aliwaambia waandishi habari katika mkutano wa pamoja na Orban.
Merkel amesema kudhibiti mipaka ya Umoja wa Ulaya sio kuunda ngome dhidi ya watu ambao wanaletwa na wasafirishaji haramu wa watu ama kupitia safari hatari katika jangwa la sahara na bahari ya Mediterania. Amesema kundi hilo la mataifa linahitaku kutia sainia makubaliano na mataifa ya Afrika kuhakikisha uhamiaji halali unawezekana.
Kwa upande wake Orban alisema Ujerumani inapaswa kushukuru kwa Hungary kujenga ukuta katika mipaka yake na Serbia na Croatia, ambao alisema unalindwa masaa 24 kwa siku na wanajeshi 8,000". Bila hivyo wakimbizi 4,000 hadi 5,000 wangekuwa wanawasili nchini Ujerumani kila siku. Huu ni mshikamano , mshikamano ambao unapaswa kuchukuliwa kwa dhati," amesema Orban.
Mazungumzo ya muungano wa serikali
Pia Merkel anatarajiwa kufanya mazungumzo leo na viongozi wa vyama vinavyounda muungano wa serikali yake vya SPD na CSU ambapo chama cha CSU kinataka makubaliano yanayotaka kuundwe kile kinachoitwa vituo vya kuwashikilia kwa muda wahamiaji karibu na mpaka wa kusini wa Ujerumani .
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer , wakati huo huo, anakutana na kansela wa Austria Sebastian Kurz kufanya majadiliano kuhusu makubaliano ambayo yatashuhudia Austria ikiwarejesha wahamiaji ambao hawataweza kuingia nchini Ujerumani. Akizungumza bungeni leo Seehofer alisema.
"Mwanzoni mwa wiki tulifikia makubaliano baada ya mjadala mkali katika vyama ndugu, na ninaamini kabisa kwamba tutafikia makubaliano, serikali inayoaminika pamoja na mshirika wetu chama cha SPD, na hatua muhimu sana hivi sasa ni mpango wa mipaka mipya wiki iliyopita, haikuweza kueleweka kwamba watu ambao wamepigwa marufuku kuingia waliruhusiwa kuingia tena Ujerumani, kitabu hiki kimefungwa sasa. Tutapata vituo vya muda hivi sasa ambapo watu wanaoomba hifadhi watarejeshwa kule walikotoka katika nchi zile zinazohusika na wao."
Merkel amewaambia waandishi habari katika mkutano na waandishi habari mjini Berlin kwamba anataka kulinda, ubinadamu wa Ulaya, wakati ikifikia vipi wahamiaji wanavyotendewa na hicho ndio huenda kinatutenganisha, amesema Merkel.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga