Obama: Silaha za kemikali Syria ni hatari kubwa
23 Agosti 2013Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Marekani, CNN, ambayo yamerushwa mchana wa leo, Rais Barack Obama amesema kuwa madai kwamba mashambulizi hayo ya silaha za kemikali yamefanywa ni hali ya kutia wasiwasi sana, akasisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa kulipa umuhimu unaofaa suala hilo.
Alisema, ''Tulichokiona hakika kinaonyesha kuwa hili ni tukio kubwa, na lenye kuzusha wasiwasi. Tayari tumeanza mashauriano na Jumuiya ya Kimataifa, kupitia Umoja wa Mataifa tunajaribu kutafuta hatua muafaka za kuchukuliwa, na tumeitaka Syria kuwaruhusu wachunguzi wa umoja huo walioko huko kufanya uchunguzi.''
Shaka shaka kuingilia kati
Hata hivyo, katika maelezo yake Rais Obama ameashiria kuwa hayuko tayari kuiingiza moja kwa moja Marekani katika vita vya Syria, kwa hofu ya gharama kubwa inayoweza kujitokeza kifedha, na hali kadhalika maisha ya watu yanayoweza kuangamizwa.
''Ikiwa Marekani itaingilia kati nchini Syria bila ruhusa ya Umoja wa Mataifa wala ushahidi wa kutosha, yanaweza kuibuka maswali juu ya uhalali wa hatua hiyo kisheria'' amesema Obama, na kuongeza kuwa uungwaji mkono wa nchi nyingine kwa hatua hiyo ni suala jingine ambalo lazima litiliwe maanani.
Obama amesema kwamba dhana kuwa Marekani peke yake inaweza kutatua mgogoro wa Syria wenye unaoambatana na matatizo makubwa za kimadhehebu na kikabila, ni kupotosha ukweli wa mambo.
Aidha, Rais Barack Obama amemtaka rais wa Syria Bashar al-Assad kutoa ushirikiano kamili na wachunguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa, lakini akatoa tahadhari kuwa hana imani kuwa wito huo utaitikiwa.
Urusi yawatuhumu waasi
Katika kile kinachoonekana kuwa utupianaji wa lawama, Urusi imesema kuwa waasi wa Syria ndio wanaokwamisha wachunguzi hao wa silaha wa Umoja wa Mataifa kufika eneo ambako imedaiwa silaha za kemikali zilitumiwa.
Wizara ya mambo ya nchi za nje ya nchi hiyo imewashutumu waasi ambao ndio wanaothibiti eneo hilo la mashambulizi, kukwamisha kwa makusudi uchunguzi usioegemea upande wowote kuhusu madai yao. Hali kadhalika, katika tangazo hilo la wizara yake ya mambo ya nchi za nje, Urusi imelaani miito ya matumizi ya nguvu dhidi ya serikali ya Syria kutokana na madai hayo kuwa imetumia silaha za kemikali.
''Kutokana na wimbi jipya la propaganda dhidi ya Syria, tunaamini kuwa shinikizo linalowekwa na baadhi ya nchi za Ulaya kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha matumizi ya nguvu, halikubaliki''; limesema tangazo hilo.
Urusi imesema picha zinazoonyeshwa kama ushahidi kuwa serikali ya Syria ilitumia silaha za kemikali, ziliwekwa hata kabla ya tukio hilo kuripotiwa.
Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef