Ban aonya juu ya matumizi ya silaha za kemikali Syria
23 Agosti 2013Wasiwasi wa Ban Ki-moon unatokana na ripoti zinazosema kwamba silaha za kemikali huenda zikawa zimetumika nchini Syria dhidi ya raia wake.
Akizungumza wakati alipokuwa ziarani Korea ya Kusini, Ban alisema matumizi ya silaha hizo mahali popote yanaashiria uvunjaji wa sheria za kimataifa na wale watakaopatikana na kosa hilo la uhalifu wanapaswa kukabiliwa na mkono wa sheria.
Muungano wa Upinzani wa Syria umesema kwamba siku ya Jumatano utawala wa Bashar al-Assad uliwaua takriban watu 1, 300 baada ya kurusha gesi za sumu katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi nje ya mji wa Damascus, madai ambayo serikali imeyakana vikali.
Wakati huo huo, Urusi imeiomba Syria kushirikiana na wachunguzi wa UN wanaokumbana na changamoto ya kufanya uchunguzi wao.
Kulingana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov na mwenzake wa Marekani John Kerry, wamekubaliana kuwa uchunguzi unapaswa kufanyika juu ya madai ya kutumika silaha hizo za kemikali. Serikali ya Assad imekubali wachunguzi hao kuingia tu katika eneo la Khan Al-Assal na sio maneo mengine.
Waasi waombwa kulihakikishia kundi la wachunguzi
Taarifa pia kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imewataka waasi wa Syria kuahidi usalama wa kundi hilo la wachunguzi wa Umoja wa Mataifa. Urusi imekuwa mshirika mkubwa wa Assad hasa wakati huu ambapo Syria inakabiliana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya kemikali wa Umoja wa Mataifa, Hamish De Bretton, amesema ni kwa uchunguzi huru tu, ndipo ukweli utakapojuilikana, ingawa hali ya usalama inatisha
"Iwapo wataweza kufika huko, manake kwa sasa sio salama sana kutokana na mashambulizi yanayoendelea, lakini wakiwezeshwa kufíka huko wana vifaa maalum vinavyoweza kubaini iwapo silaha za kemikali zilitumika na ni kemikali ya aina gani ambayo itawezesha kujua ni kina nani hasaa waliotumia silaha hizo," Alisema Bretton.
Idadi ya wakimbizi watoto wa Syria inapanda na kufikia milioni moja.
Huku hayo yakiarifiwa Umoja wa Mataifa umesema idadi ya watoto wakimbizi kutoka Syria waliosajiliwa sasa imefikia milioni moja.
Shirika hilo limesema nusu ya wakimbizi milioni mbili wanaokimbia mapigano nchini humo ni watoto huku 740,000 wakiwa chini ya miaka 11.
Antonio Guterres, mkuu wa shirika la watoto linalowashughulikia wakimbizi UNHCR amesema hata baada ya watoto hawa kukimbia Syria na kuingia katika maeneo salama, huwa bado wanakumbwa na mshituko, wana mawazo mengi na wanahitaji watu wa kuwatuliza akili na kuwapa matumaini.
Wakimbizi wengi wanaotokea Syria wanaingia nchini Lebanon, Jordan, Uturuki, Iraq, na Misri.
Hata hivyo maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema sasa wakimbizi wengine wengi wanakimbilia Kaskazini mwa Afrika na Bara Ulaya.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef