NATO yashambulia tena mji wa Tripoli
17 Mei 2011Makazi ya Gaddafi mjini Tripoli yameonekana katika hali mbaya, jengo la huduma za usalama na makao makuu ya wakala wa kukukabiliana na rushwa nchini Libya yameshambuliwa kwa makombora na ndege za NATO mapema leo.
Jana huko mjini The Hague, mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita, ICC Luis Moreno-Ocampo aliomba kutolewa kwa waranti ya kukamatwa kwa Gaddafi na mtoto wake Seif al- Islam akimjumuisha mkuu wa usalama, Abdullah Senusi kwa tuhuma ya uhalifu dhidi ya binaadamu.
Mwendesha mashitaka huyo wa Kiajentina amesema kuna ushahidi " kwamba Moammar Gaddafi binafsi ameamuru mashambulizi ya raia wa Libya wasio na hatia."
Jopo la majaji wa ICC watakutana kujadili endapo watakubali au kulikataa ombi hilo la kumtia nguvuni Gaddafi.
Moreno Ocampo amesema maelfu ya watu wameuwawa na kiasi ya watu laki 7.5 wamelazimika kuikimbia nchi hiyo tangu Gaddafi alipoamuru wanajeshi wake kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakipinga utawala wake wa kidikteta wa miongo minne.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague ametoa wito wa jumuiya ya kimataifa kuuinga mkono kwa hali na mali ICC huku akisema amelipokea vyema tangazo hilo.
Waasi nao mjini Benghazi, wameipokea kwa shangwe kauli hiyo ingawa wamesema Gadhafi angepaswa kushitakiwa nchini Libya kwanza.
Serikali ya Libya imelalamika kwa kusema mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya ICC anatekeleza majukumu yake kwa kutumia taarifa zisizoeleweka. Msemaji wa serikali ya Libya Musa Ibrahim amesema tangu kuanza kwa mgogoro nchini humo, ICC imekuwa ikipata taarifa zake kwa kutegemea ripoti za vyombo vya habari.
Katika uwanja wa mapambano, majengo mawili ya kumbi za kitaifa za Al Jamhuriya, karibu na makazi ya Gaddafi yameshambiliwa mapema leo.
Hata hvyo muda mfupi baadae vikosi vya kukabiliana na moto vilionekana vikifanya jitihada za kuuzima moto huo.
Msemaji wa serikali, Mussa Ibrahim alidai Baraza la Mpito la Waasi limevielekeza vikosi vya NATO kulishambulia jengo la wakala wa kukabiliana na rushwa kwa lengo la kuteketeza mafaili ya maafisa wa zamani wa utawala huo ambao wamejiunga na upande wa waasi ambao pia wanatuhumiwa kwa rushwa.
Milipuko mingine mitatu ilisikika jana katika eneo hilo hilo. Baadhi ya maeneo ya Tripoli yamekuwa yakishambuliwa karibu kila siku tangu kuanza kutekelezwa kwa azimio la umoja wa mataifa la kuzuia ndege kuruka katika anga ya Libya na kuwalinda raia mnamo Machi 19 mwaka huu.
Mwandishi: Sudi Mnette/ AFP
Mhariri:Josephat Charo