1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kuujadili usalama wa Ukraine waahirishwa

Angela Mdungu
9 Oktoba 2024

Mkutano wa usalama wa Ukraine uliopangwa kufanyika katika kambi ya jeshi la Marekani ya Ramstein iliyo Ujerumani, umeahirishwa baada ya Rais Joe Biden kuifuta safari yake nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/4laWy
Biden na Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Joe Biden wa MarekaniPicha: AFP

Biden aliifuta safari yake ya Ujerumani Jumanne kutokana na kitisho cha Kimbunga Milton, huko Florida.Taarifa ya Kamandi ya jeshi la Marekani ya Ramstein imesema mkutano uliopangwa kufanyika katika kambi hiyo Oktoba 12 umeahirishwa ingawa haikutoa ufafanuzi kuhusu tarehe mpya ya mkutano huo.

Uamuzi wa kuusogeza mbele mkutano huo si wakushangaza kwani umetolewa muda mfupi baada ya Biden kusema Jumanne kuwa asingeweza kufanya ziara Ujerumani kama ilivyopangwa.  

Ameahirisha safari hiyo, nchi yake ikikabiliwa na kimbunga kikali kinachoelekea katika maeneo kadhaa ikiwemo Florida ambako uharibifu mkubwa umesababishwa na kimbunga Helene kilichopiga hivi karibuni. Biden alitarajiwa kuwasili Berlin Alhamisi kukutana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz pamoja na Rais Frank-Walter Steinmeier.

Mkutano uliopaswa kufanyika Ramstein ungehudhuriwa na mataifa mengine 50 washirika wa Ukraine  ili kujadili namna ya kuisaidia kijeshi nchi hiyo. Rais Volodymyr Zelensky alitarajiwa pia kuwa sehemu ya majadiliano hayo.

Mara ya mwisho Zelensky, alihudhuria mkutano katika kambi hiyo mwezi Septemba ambapo alishinikiza Kyiv ipewe silaha zaidi ili kupambana na vikosi vya Ukraine na kutaka akubaliwe kufanya mashambulizi zaidi ya kijeshi ndani zaidi mwa Urusi kwa kutumia silaha za masafa marefu zilizotolewa na nchi washirika.

Zelensky ahudhuria mkutano wa nchi za Balkan katika juhudi za kutafuta amani   

Wakati huohuo, Rais wa Ukraine  Volodymyr Zelensky amewasili  Croatia katika mkutano wa viongozi wa mataifa ya Balkan wakati nchi yake ikishinikiza kupewa misaada zaidi ili kupambana na Urusi.  Zelensky ametangaza kuwasili Croatia na kusema kuwa mkutano huo utajadili juhudi za kimataifa za kujaribu kurejesha amani pamoja na ushirikiano na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Daniel Roland/AFP/Getty Images

Kwa upande wake Urusi kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni Maria Zakharova imesema kuwa, Ukraine haitapata amani kama itajiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Ameongeza kuwa kile Moscow inachokiita operesheni maalumu ya kijeshi Ukraine ilikuwa ni majibu ya Jumuiya hiyo kutaka kujitanua.

Katika hatua nyingine, Shirika la Habari la Urusi RIA limearifu kuwa wanajeshi wa Urusi wamefanikiwa kuvikomboa vijiji vya Novaya  Sorochina  na Pokrovsky kutoka katika udhibiti wa Ukraine kwenye mkoa wa Magharibi wa Kursk.

Wanajeshi wa Urusi wamekuwa wakipambana kuviondoa vikosi vya Ukraine kutoka Kursk tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti baada ya Kyiv kufanya uvamizi wa kushtukiza katika eneo hilo la mpakani.