Urusi yaushambulia mji wa Lviv magharibi mwa Ukraine
5 Septemba 2024Urusi imeushambulia mji wa Lvivmagharibi mwa Ukraine siku ya Jumatano, na kuwaua watu saba wakiwemo watoto na kuharibu majengo ya kihistoria. Miongoni mwa waliokufa ni watu wanne kutoka familia moja, mwanamke na binti zake watatu, na kumwacha baba yao akiwa manusura pekee. Meya wa jiji hilo amesema shambulio hilo la kombora pia limejeruhi watu 64 na kuharibu shule na vituo vya matibabu pamoja na majengo katika kituo cha kihistoria cha Lviv.
Shambulio hilo limefanyika wakati mawaziri kadhaa wa Ukraine, akiwemo mwanadiplomasia mkuu Dmytro Kuleba, wakijiuzulu. Rais Volodmyr Zelensky wa Ukraine amesema hatua hiyo ni sehemu ya mabadiliko ambayo yataleta nguvu mpya katika serikali. Urusi imezidisha mashambulizi yake ya anga dhidi ya Ukraine tangu Kyiv ilipoanzisha mashambulizi ya kuvuka mpaka katika eneo la Kursk nchini Urusi mwezi uliopita.