Misri, Sudan zasitisha mazungumzo na Ethiopia
5 Agosti 2020Sakata la ujenzi wa bwawa la kuzalisha nishati ya umeme linalojengwa na Ethiopia kwenye mto Nile limechukua sura mpya baada ya Misri kuamua kujiondoa kutoka katika duru ya hivi karibuni ya mazungumzo na Ethiopia. Misri imesema inakwenda kwanza kujipanga upya.
Misri imesema siku ya Jumanne kwamba imeamua kujitoa kutoka katika duru ya karibuni ya mazungumzo na Ethiopia juu ya ujenzi wa bwawa la kuzalishia nishati ya umeme litakalogharimu mabilioni ya dola za Kimarekani katika mto Blue Nile baada ya serikali ya Ethiopia kupendekeza rasimu mpya ya miongozo ya kulijaza maji bwawa hilo.
Ujenzi mpya wa bwawa kubwa la kuzalishia umeme ambalo linajengwa takribani kilometa 15 kutoka mpaka wa Ethiopia na Sudan katika mto Blue Nile imekuwa ni kitovu cha mzozo kati ya nchi tatu. Misri inahofia kuwa ujenzi wa mradi huo unaweza ukasababisha upungufu wa maji juu ya mto wakati Sudani inajali usalama wa bwawa.
Mitazamo kinzani kuhusu mradi
Lakini wakati Misri ikipinga mradi huo, wengine wanaona kuna umuhimu wa mradi huo kufanyika. "Inahitaji bwawa hilo ili kuwakwamua watu wake wengi katika lindi la umasikini. Inahitaji bwawa hilo la kuzalisha umeme ili kukuza viwanda vyake," alisema Peter Kagwanja, mtaalam wa masuala ya usalama kutoka Kenya.
Soma zaidi Waethiopia waandamana kulishangilia bwawa la umeme
Mto Blue Nile ni tawi la mto Nile ambapo watu milioni 100 huko nchini Misri wanapata asilimia 90 ya maji yao safi kutoka katika mto Nile.
Serikali ya Cairo ilisema Ethiopia iliwasilisha ombi siku ya Jumanne kwamba imetengwa katika miongozo ya kufanya kazi na utaratibu wa kisheria wa kusuluhisha mabishano.
Hofu juu ya mazungumzo
Wizara ya umwagiliaji ya Sudan imesema msimamo uliowasilishwa hivi karibuni katika mazungumzo siku ya Jumanne ulizua hofu kubwa juu ya mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea kuhusiana na sakata hilo la ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalishia nishati ya umeme.
Soma zaidi Ethiopia, Misri, Sudan zakubali kuahirishwa ujazaji wa bwawa la Nile
Waziri wa umwagiliaji wa Ethiopia Seleshi Bekele alielezea matumaini ya juu ya mazungumzo na aliandika kwenye mtandao wake wa twiter siku ya jumanne akisema kuwa Ethiopia ingependa kutia saini makubaliano ya kwanza ya kulijaza maji bwawa lake mapema na pia kuendeleza mazungumzo kukamilisha mazungumzo kamili katika vipindi vifuatavyo.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema mapema Julai mwaka huu
kwamba nchi yake tayari ilifanikisha malengo yake ya mwaka wa kwanza
ya kulijaza bwawa hilo, kutokana hasa na msimu wenye mvua za kutosha.
Chanzo: Reuters