Ethiopia kutoshiriki duru ya mwisho ya mazungumzo ya Nile
26 Februari 2020Wizara ya maji ya Ethiopia imesema hayo siku ya Jumatano. Makubaliano ya mwisho kuhusu mradi wa bwawa kubwa kabisa la umeme yalitarajiwa kufikiwa mwezi huu, lakini waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema kwenye ziara yake wiki iliyopita nchini Ethiopia kwamba makubaliano hayo sasa yanaweza kuchukua miezi kadhaa kwa kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanywa. Ethiopia haitashiriki mazungumzo hayo yanyofanyika mjini Washington kesho Alhamisi na Ijumaa kwa sababu ujumbe wa nchi hiyo haujahitimisha uchunguzi wake na wadau muhimu, hii ikiwa ni kulingana na wizara hiyo ya maji, umwagiliaji na nishati kupitia ukurasa wake wa Facebook. Imesema, tayari wamemuarifu waziri wa fedha wa Marekani kuhusiana na hatua hiyo. Tayari ujumbe wa Sudan umewasili nchini Marekani kwa ajili ya mazungumzo hayo.