Maafisa wa Misri, Ethiopia na Sudan kukutana Marekani?
23 Oktoba 2019Kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Misri, mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Ethiopia na Sudan ambayo ndiyo mataifa matatu yanayoathirika moja kwa moja na mradi huo, utafanyika mjini Washington.Wizara hiyo lakini haikutaja tarehe utakapofanyika mkutano huo wala haikueleza pia iwapo hizo nchi zengine zimekubali kuhudhuria.
Misri ina hofu kwamba mradi huo mkuu wa bwawa unaoendeleakatika mpaka wa Ethiopia na Sudan utapunguza kiasi cha maji yanayotiririka Misri kutoka kwenye mto Nile ambao Misri inautegemea kwa karibu kila shughuli zake.
Mradi utakamilishwa kwa njia ambayo haitaidhuru nchi yoyote
Waziri Mkuu wa Ethiopia aliyeshinda tuzo ya amani ya Nobel hivi majuzi Abiy Ahmed ameonya kwamba iwapo kuna haja ya kuingia katika vita kuhusiana na mradi huo wa bwawa, nchi yake inaweza kukusanya mamilioni ya watu kwa ajili ya vita hivyo na Misri imesema imeshtushwa na matamshi hayo. Abiy lakini amedai kuwa mazungumzo ndiyo njia ya pekee itakayosuluhisha mkwamo uliopo.
"Mradi huu utakamilishwa kwa njia ambayo nchi zilizo chini ya mto huu hazitaathirika. Waethiopia hawana nia ya kuwadhuru wa Wamisri badala yake wanataka tu kunufaika kutokana na bwawa hilo," alisema Abiy Ahmed.
Waziri huyo Mkuu ameyasema haya wakati wa kikao cha kuuliza na kujibu maswali bungeni. Hii leo Abiy Ahmed anatarajiwa kukutana na Rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika katika mji wa Sochi nchini Urusi.
Bwawa ni muhimu kwa ustawi wa Ethiopia
Mazungumzo kuhusiana kutatua utata uliopo katika ujenzi wa bwawa hilo linalogharimu dola bilioni tano yalifeli mapema mwezi huu. Bwawa lenyewe kwa sasa lemejengwa hadi kufikia asilimia sabini na linatarajiwa kusambaza umeme kwa idadi ya Waethiopia milioni mia moja.
Ethiopia inasema bwawa hilo ni muhimu kwa ustawi wake kiuchumi na imekanusha kwamba mazungumzo yamesita na kuituhumu Misri kwa kujaribu kuuendea kinyume mchakato huo.
Vyombo vya habari vinavyoiunga mkono serikali nchini Misri vimelifanya jambo hilo kuwa kitisho cha usalama wa kitaifa na kudai kwamba huenda likapelekea hatua za kijeshi kuchukuliwa.